Pesa za ‘Nyota’ si za kuoa, vijana waambiwa
GAVANA wa Samburu Laiti Lelelit, jana alitumia hafla iliyohudhuriwa na Rais William Ruto kuwaonya vijana dhidi ya kutumia pesa za mradi wa NYOTA kuoa.
Bw Lelelit aliwaambia vijana watumie pesa hizo kuanzisha miradi ya kuzalisha mapato badala ya kuandaa harusi au mahitaji mengine ya kibinafsi.
“Najua vijana wetu mnapenda kuoa. Hii pesa si ya kuenda kuoa. Ule mrembo uko naye mwambie wacha tufanye biashara mambo ikiwa vizuri tufanye harusi,” akasema Bw Lelelit.
Rais Ruto alikuwa amehudhuria hafla ya kutoa hela NYOTA katika eneo la Archer Post Samburu. Gavana huyo alisema hela hizo ni za kuinua mapato ya vijana na zinastahili kutumiwa kwa hekima.
Wakati huo huo, Kaunti ya Meru imelaumiwa kwa kukosa magari ya zimamoto yanayosaidia kupambana na visa vya moto vinavyotokea mara kwa mara na kusababisha uharibifu mkubwa wa mali.
Mnamo Januari 4, moto mkubwa ulizuka katika Gereza la Meru na licha ya Kituo cha Zimamoto Meru kuwa umbali wa kilomita mbili pekee, hakuna msaada wowote ambao ulipatikana kutoka kituo hicho.
Askari wanaohudumu gerezani walisaidiana na wenyeji kuzima moto huo wakitumia ndoo ambazo walijaza maji, mchanga na matawi ya miti.
Mara nyingi kaunti ikituma gari na wahudumu kukabiliana na visa hivyo, wao hufika kama wamechelewa na hufurushwa na wakazi.
Serikali ya Kaunti ya Meru imekiri kuwa hali ni mbaya kiasi kwamba wamekuwa wakitegemea magari ya zimamoto kutoka kaunti jirani ya Tharaka-Nithi.
Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Kupambana na Majanga Kaunti ya Meru, Bi Lena Kiambi, alisema kaunti ilikodisha magari sita ya zimamoto lakini yote yamekwama na yapo katika karakana.
“Nilipoingia afisini, nilipata magari yote yakiwa katika hali mbaya na mawili hayawezi kufanya kazi kabisa hata yakitengenezwa. Kuna magari mawili ya kuzima moto yaliyotengenezwa lakini huharibika mara kwa mara na hutumika kwenye miji ya Meru na Maua,” akasema Bi Kiambi.
Kaunti ya Meru ina vituo vitatu vya moto ambavyo vinapatikana Meru, Maua na Timau. Gari la zimamoto la Maua limeegeshwa tu huku lile la Timau bado linasubiri kukarabatiwa.
“Kuhusu visa vitano ambavyo huripotiwa kila wiki, Timau na Maua ndizo huvishuhudia visa vingi vya moto ilhali ni gari moja la kuzimamoto ndilo linafanya kazi,” akaongeza Bi Kiambi.