Pigo kwa mbakaji korti ikidumisha kifungo cha miaka 30
MFUNGWA mmoja amepata pigo baada ya Mahakama Kuu kukataa kupitia upya kifungo cha miaka 30 alichopewa kwa kosa la ubakaji wa mtoto katika Kaunti ya Kilifi.
Safari Kwicha alidai kuwa wahalifu wote wa makosa kama yake waliohukumiwa chini ya sheria za adhabu za chini zisizobadilika wanapaswa kuzingatiwa katika kupunguziwa adhabu zao.
Aliomba mahakama ipitie upya kifungo chake baada ya rufaa yake ya awali kutupiliwa mbali na Mahakama Kuu ya Malindi.
Hata hivyo, Jaji Mugure Thande alikataa ombi lake, akisema kuwa mahakama yake haina mamlaka ya kufungua upya kesi ambayo rufaa yake tayari ilikuwa imetolewa uamuzi.
Alisisitiza kuwa mahakama inaweza tu kutumia mamlaka iliyopewa waziwazi na Katiba au sheria.
Jaji Thande alifafanua kwa kuwa Kwicha tayari alishindwa katika rufaa yake dhidi ya hukumu na kifungo chake mbele ya Mahakama Kuu, suluhisho lake pekee la kisheria lilikuwa ni kukata rufaa katika Mahakama ya Rufaa.
Alieleza kuwa Mahakama Kuu haina mamlaka ya kupitia upya uamuzi wake katika suala kama hilo.
Jaji huyo alihitimisha kuwa ombi la Kwicha, lililowasilishwa Januari 25, 2024, halina msingi kwa sababu ya ukosefu wa mamlaka, na hivyo akalitupilia mbali
Kwicha alihukumiwa kwa kosa la kumbaka mtoto na akapewa kifungo cha miaka 30 jela.
Rufaa yake ya awali katika Mahakama Kuu ilitupiliwa mbali, na kifungo chake kuthibitishwa.
Hata hivyo, Kwicha bado ana nafasi ya kuwasilisha malalamiko yake katika Mahakama ya Rufaa.