Habari Mseto

Pigo kwa wanaokaa mtaa wa kifahari wa Kizingo korti ikiruhusu jumba la orofa 16

May 15th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA BRIAN OCHARO

WAKAZI wa mtaa wa kifahari wa Kizingo mjini Mombasa wamepata pigo baada ya mahakama kuruhusu ujenzi wa jumba la ghorofa 16 karibu na nyumba zao.

Kampuni ya Khansa Developers Ltd sasa itaendelea na mradi ambao ulikuwa umekwama baada ya wakazi wa eneo hilo kuibua pingamizi kwa msingi kwamba faragha yao itaingiliwa ikiwa jengo hilo litaruhusiwa kujengwa.

Jaji wa Mahakama ya Mazingira na Ardhi Lucas Naikuni aliiruhusu kampuni hiyo kuendelea na mradi huo, lakini kwa masharti kwamba orofa zitapunguzwa kutoka 18 hadi 16.

“Tamko limetolewa kwamba mapendekezo ya ujenzi wa jengo la orofa 18 katika ardhi numbari Mombasa/ Block/XXVI595 ipunguzwe hadi orofa 16 kwa mujibu wa sheria,” Jaji huyo alisema.

Hata hivyo, Jaji huyo aliagiza kampuni hiyo kuwasilisha upya ombi la kuidhinishwa kwa mradi hiyo kwa kaunti na Mamlaka ya Kitaifa ya Kusimamia Mazingira.

Pia, mahakama ilisema kuwa wananchi wote na wakazi wanaoishi katika eneo hili washirikishwe kikamilifu kuhusu mradi huo na athari zake na hatua za usalama ziwekwe wazi.

Mahakama pia imeagiza kwamba Ripoti ya Tathmini ya Athari kwa Mazingira ifanywe ili kuzuia usumbufu wa vumbi na kelele utakaosababisha na ujenzi huo.

Pia, kampuni hiyo iliagizwa kuhakikisha kuwa hakuna ongezeko la trafiki ya magari na ongezeko la mahitaji ya maji na usambazaji wa umeme.

“Khansa Developers Ltd kuhakikisha kuwa jengo hilo halipaswi kuwa tishio na pia kukiuka au kunyima wakazi haki ya mazingira safi na yenye afya na ya faragha haihatarishiwi,” alisema jaji huyo.

Katika uamuzi uliotolewa mwaka jana, Jaji Naikuni alisitisha ujenzi wa jengo hilo la orofa 18 baada ya kukubaliana na wakazi wa Kizingo kwamba jengo hilo refu lingevuruga faragha yao katika vyumba vya kulala na mabwawa ya kuogelea.

Wamiliki wa eneo la Kizingo, wakiongozwa na Mohamed Abdalla, Salim Said, Abdulaziz Abbas, Bharat Devidas, na Ketan Doshi, waliwasilisha kesi hiyo wakilalamikia kwamba haki yao ya faragha itaingiliwa pakubwa iwapo jengo hilo litajengwa.

Walisema kuwa maendeleo hayo yanafanywa kinyume na sheria na bila kujali ustawi wa wakazi wa eneo hilo na masuala ya mazingira.

Waliishtaki kampuni ya Khansa Development Limited, Ramesh Chandra Haria, Serikali ya Kaunti ya Mombasa na Nema.

Hata hivyo, kampuni hiyo ilijitetea kwa kueleza kuwa aliomba na kupata kibali cha kubadilisha matumizi ya ardhi kutoka kwa kaunti baada ya kushirikisha wananchi na kufuata taratibu sahihi za kisheria.