PNU yaahidi kujiimarisha tayari kwa uchaguzi mkuu wa 2022
Na MAGDALENE WANJA
CHAMA cha kisiasa cha Party of National Unity (PNU) kimetangaza mipango yake mikuu ya kujifufua kisiasa kwa mtayarisho ya uchaguzi wa mwaka 2022.
Hii inafuatia mkutano ulioandaliwa Kasarani mwishoni mwa wiki jana.
Chama cha PNU kinajivunia kumwezesha Rais mstaafu Mwai Kibaki kushinda uchaguzi wa mwaka 2007 kwa kipindi chake cha pili.
Chama hicho kiliundwa kwa ushirikiano wa vyama vingine kama vile KANU, Narc-Kenya, Ford-Kenya, Democratic Party, Shirikisho na National Alliance Party of Kenya.
Akizungumza baada ya mkutano, mwenyekiti wa Kamati Kuu ya Kitaifa – National Executive Committee – (NEC), David Kamau alisema kuwa chama hicho kiko imara na kitakuwa na mgombeaji wa urais mnamo mwaka 2022.
“Chama hiki kina historia ya kutoa viongozi wakuu na tayari tumeanza matayarisho ili kukirejeshea sifa yake ya hapo awali,” alisema Bw Kamau.
Aliongeza kuwa chama hicho sasa kitashiriki katika chaguzi zote nchini ikiwemo uchaguzi mdogo.
Hata ingawa chama hicho kimesalia imara wakati vyama vingine viliungana, Bw Kamau alisema kuwa wanaunga mkono ushirikiano wa Rais Uhuru Kenyatta na aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga katika salamu za Machi 9, 2018, maarufu kama ‘handshake’.