Habari Mseto

Polisi aliyemtumia Alai picha za Wakenya waliouawa na Alshabaab taabani

June 20th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na RICHARD MUNGUTI

AFISA wa polisi aliyefikishwa kortini Alhamisi akidaiwa alimtumia mwanablogu Robert Alai picha za maafisa wa polisi wanane waliofariki katika shambulizi kaunti ya Wajir Juni 15, 2019  atazuiliwa kwa siku 15 kuhojiwa.

Hakimu mkazi Bi Sinkiyian Tobiko aliamuru Inspekta Wilfred Kimaiyo azuiliwe na maafisa wa kitengo cha kupambana na ugaidi ATPU kwa siku 15.

“Polisi wanahitaji muda kukamilisha mahojiano pamoja na kukagua orodha ya simu zilizopokewa na kupigwa katika nambari ya afisa huyu wa usalama,” alisema Bi Tobiko.

Hakimu alitoa agizo hilo alipokubalia ombi la Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) kupitia kwa wakili wa Serikali Bi Angela Odhiambo.

Wakili Marcelino Lesaigor aliyemwakilisha Insp Maiyo. Picha/ Richard Munguti

DPP aliiomba mahakama imzuilie Insp Maiyo kwa siku 15 kuwezesha wachunguzi kufanya mahojiano na mshukiwa huyu anayeshukiwa kuwa na uhusiano na mmoja wa magaidi waliotekeleza shambuli hilo.

“Naomba Insp Maiyo azuiliwe kwa siku 15 kuhojiwa na maafisa wa kupambana na ugaidi,” alisema Bi Odhiambo.

Hakimu mkazi mahakama ya Milimani Nairobi Bi Sinkiyian Tobiko alifahamishwa kuwa Insp Maiyo alikuwa akiwasiliana na Bw Alai aliyezuiliwa kwa siku 14 Jumatano kuhojiwa na maafisa wa polisi wa kitengo cha ugaidi ATPU.

Hakimu aliombwa aamuru afisa huyo wa usalama azuiliwe kusaidia maafisa wa upelelezi kubaini kilichojiri.

“Uchunguzi uliofanywa kufikia sasa unabaini nambari ya simu ya Insp Maiyo ilipigiwa watu waliokuwa eneo la shambulizi Wajir na pia nchini Somalia,” Bi Odhiambo alimweleza hakimu.

Kiongozi wa mashtaka Angela Odhiambo. Picha/ Richard Munguti

Bi Odhiambo alisema maafisa wa polisi wa kupambana na uhalifu wa kimitandao watachunguza orodha ya simu zilizopigwa kutoka kwa nambari ya Insp Maiyo na wale aliowapigia ndipo “ibainike jinsi shambulizi hilo lilivyotekelezwa.”

Lakini wakili Marcelino Lesaigor alipinga ombi hilo la DPP akisema “ hakuna ushahidi uliowasilishwa dhidi ya mshukiwa aliyehudumu akiwa afisa wa usalama kwa miaka 20 kuwezesha korti kumzuilia.”

Bw Lesaigor alisema Maiyo alijisalamisha kwa maafisa wa ATPU na wala hakutiwa nguvuni.

“Badala ya kumzuilia Maiyo anapasa kuachiliwa akamuomboleze mmoja wa maafisa wa polisi aliyeaga wakati wa shambulizi hilo la Juni 15 2019 ambapo maafisa wanane wa usalama walipoteza maisha yao,” alisema Bw Lesaigor.

Hakimu mkazi Bi Sinkiyian Tobiko. Picha/ Richard Munguti

Hakimu aliamuru Insp Maiyo azuiliwe akitayariasha uamuzi iwapo ataamuru Insp Maiyo azuiliwe kuwasaidia maafisa wa ATPU na wale wa uhalifu wa kimitandao kukamilisha uchunguzi.

Bi Tobiko alifahamishwa Alai na afisa wa idara ya magereza Patrick Safari wanaodaiwa walikuwa wanawasiliana na magaidi Wajir walizuiliwa kwa siku 14.

Mahakama ilifahamishwa nambari za simu za watatu hao zitachunguzwa kubaini uhusiano wao na magaidi waliotekeleza shambulizi hilo ama washirika wao.