Polisi miongoni mwa abiria 11 waliouawa na magaidi
Na BRUHAN MAKONG
MAAFISA tisa wa polisi ni miongoni mwa watumishi 11 wa umma waliouawa kwenye shambulizi la kigaidi wakiwa katika basi eneo la Kotulo, Wajir.
Shambulizi hilo lilitekelezwa na magaidi wanaoshukiwa kuwa wanachama wa kundi la al-Shabab kati ya Kutulo na Wargadud na waliouawa ni watumishi wa umma.
Watu sita walinusurika wakiwa na majeraha madogo wakati wa shambulio hilo ambalo serikali ililaani.
“Rais angependa kulifahamisha taifa kwamba vikosi vya usalama vinawasaka wauaji hao na anatoa hakikisho kwamba serikali haitalegea katika kuwasaka vikali wahalifu ikiwemo washukiwa wa ugaidi katika kutimiza wajibu wake wa kipekee wa kulinda maisha na mali ya Wakenya,” ilisema taarifa kutoka Ikulu.
Kamanda wa polisi katika Kaunti ya Wajir, Stephen Ng’etich, alisema magaidi hao waliwalenga watu wasio wakazi wa eneo la Kaskazini Mashariki.
Alisema waliwatenga na abiria wengine na kuwaua kabla ya kuruhusu dereva kuendelea na safari kuelekea Mandera.
Hata hivyo, dereva wa basi alikatiza safari na kurejea katika kituo cha polisi cha Kotulo.
Bw Ng’etich alisema wengi wa waliouawa walikuwa maafisa wa kikosi cha kupambana na wezi wa mifugo waliokuwa wakirejea katika kambi zao eneo la Elram, Kaunti ya Mandera.
Alisema maafisa hao waliwasili Wajir mnamo Ijumaa kutoka Nairobi na kupanda basi siku hiyo adhuhuri.
Ilisemekana kuwa mmoja wa raia wawili waliouawa alikuwa daktari. Awali iliripotiwa kuwa maafisa wawili wa polisi hawakujikana waliko baada ya shambulio hilo lakini Jumamosi polisi walitangaza kuwa walipatikana kichakani wakiwa hai.
Shambulizi hilo lilijiri mwezi mmoja baada ya magaidi hao kushambulia kituo cha polisi cha Dadajabula, Wajir kuokoa wenzao wawili waliokuwa wakizuiliwa humo. Wiki mbili zilizopita, maafisa wa polisi walishambuliwa kwa kilipuzi wakisafiri kutoka Mandera kwenda Wajir.
Miaka mitano iliyopita watu 28 wasio wakazi wa eneo hili waliuawa katika shambulio kwenye basi sawa na la Ijumaa. Viongozi mbali mbali walilaani shambulio hilo na kuwataka Wakenya kuungana kuangamiza ugaidi.
Rais Kenyatta alionya kuwa wanaoendeleza ugaidi nje na ndani ya Kenya hawatavumiliwa.