Polisi wachunguza kifo cha mwenzao aliyejipiga risasi
Na GEORGE SAYAGIE.
POLISI mjini Narok bado wanachanganua taarifa kubaini hali inayozingira kujiua kwa afisa wa GSU aliyefanya kazi katika ofisi ya Mkuu wa Polisi Joseph Boinnet.
Kamanda wa Polisi wa Kaunti ya Narok Thomas Ngeiwua, jana alithibitisha kuwa Bw Anthonu Lemayan, mwenye miaka 45, aliyejipiga risasi akiwa Narok Jumapili iliyopita, alikuwa mmoja wa madereva katika afisi ya Bw Boinnet.
Bw Ngeiwua alisema afisa huyo atazikwa Desemmba 17, nyumbani kwake Kisirir, huku uchunguzi kuhusu kiini cha kujitia kitanzi ukiendelea.
“Hakuwa dereva wa kibinafsi wa Mkuu wa Polisi lakini laifanya kazi katika ofisi yake na uchunguzi wetu unaonyesha kuwa alikuwa kwa likizo akiwa mgonjwa wakati tukio hilo lilitokea katika mataa wa Mwamba mjini Narok,” akasema.
Aliongeza kuwa nduguye marehemu alirekodi taarifa kwa polisi siku hiyo akisema nduguye alikuwa likizoni.
“Kwenye ripoti ya kitanzi, mtu aliyejitambulisha kama nduguye; Evans Leteipa Maasai alithibitisha kuwa nduguye alijiua katika mtaa wa Mwamba mjini Narok,” akasema na kuongeza kuwa mwili wa mwendazake uko katika chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospitali ya Kaunti ya Narok ukisubiri kufanyiwa upasuaji wa uchunguzi.
Alisimulia kuwa polisi ambao walikimbia kwa eneo la kitanzi walipata mwili wake ukiwa na majeraha ya risasi chini ya kidevu na kichwani.
Pia walipata bastola, risasi iliyotumika na risasi zingine 14. Hata hivyo, hakuacha karatasi yoyote yenye maandishi ya sababu ya kujiua.
Mtu wa familia yake alifichua kuwa afisa huyo alikuwa amehusika katika ajali ya barabarani mwaka jana ambayo ilimletea maradhi ya kichwa na bado alikuwa akitumia dawa.
Kulingana na Bw Ngeiwua, haieleweki jinsi afisa huyo alipewa bastola licha ya kuugua akili.