• Nairobi
  • Last Updated May 13th, 2024 5:30 PM
Polisi wachunguza kilichosababisha seneta kuugua

Polisi wachunguza kilichosababisha seneta kuugua

Na MARY WANGARI

POLISI wameanzisha uchunguzi katika kisa ambapo Seneta wa Machakos, Boniface Mutinda Kabaka alianza kuugua ghafla na kulazwa katika hospitali ya Nairobi Hospital.

Kulingana na mke wa seneta huyo, Bi Jennifer Mueni Kabaka aliyeandikisha taarifa kwa polisi Alhamisi, alipokea simu kutoka kwa mhudumu wa afisi ya seneta huyo, Bw Boniface Mutinda, aliyemfahamisha kuwa mume wake alikuwa amekimbizwa hospitalini na kulazwa akiwa hali mahututi.

Bi Kabaka alienda hospitalini humo akiwa ameandamana na jamaa wengine wa familia akiwemo mke mwenza-wake, Bi Vascoline Katanu Kabaka, ambapo walitambua kuwa seneta huyo alipelekwa hospitalini akilalamika kuhusu maumivu makali ya kichwa alipokuwa katika jumba lililo mtaa wa Kilimani, Nairobi.

Aliripoti kisa hicho kwa polisi na kuandikisha taarifa ambapo wapelelezi kutoka Idara ya Kukabiliana na Uhalifu (DCI) walizuru chumba ambapo seneta huyo alikuwa alipoanza kuugua. Kulingana na taarifa ya polisi iliyoonekana na Taifa Jumapili, mwanasiasa huyo alikuwa na mwanamke aliye mkazi wa eneo la Wote alipoanza kuugua.

Mwanamke huyo aliyehojiwa na wapelelezi alisema seneta huyo alianza kulalamika kuhusu kuumwa na kichwa walipokuwa chumbani na kumtuma kwenda kumnunulia dawa.

“Katika eneo hilo, mwanamke huyo alipatikana na kuwafahamisha wapelelezi kwamba alikuwa na seneta chumbani humo alipoanza ghafla kulalamika kuhusu maumivu makali ya kichwa na kumwagiza amtafutie dawa za kupunguza maumivu. Maumivu yalizidi na akafahamisha usimamizi ambao uliita ambulensi na kumkimbiza hospitalini,” ikasema taarifa.

Bw Kabaka alipozidiwa na maumivu ya kichwa ndipo mwanamke huyo akafahamisha wasimamizi wa jumba hilo ambao waliita ambulensi na kumkimbiza Nairobi Hospital.

Chumba hicho kilitengwa kwa shughuli ya uchunguzi huku ushahidi uliopatikana eneo hilo ukipelekwa katika maabara ya serikali kwa uchunguzi zaidi.

“Maafisa wa DCI walizuru eneo hilo. Seneta huyo angali amelazwa ICU. Mwanamke huyo alipelekwa katika Kituo cha Polisi cha Kilimani kwa mahojiano zaidi. Habari zaidi zitafuatia,” ilisema taarifa hiyo.

  • Tags

You can share this post!

Wakili aliyejisalimisha ICC asalia pweke Kenya ikijitenga

JAMVI: Makonde ya Joho na Mvurya yaongezeka kura za...