Habari Mseto

Polisi wageukia Safaricom kupata taarifa kumshtaki mwanahabari

May 16th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na RICJARD MUNGUTI

POLISI hawajakamilisha kuchunguza kesi dhidi ya mwanahabari anayeshukiwa alihusika na shambulizi la mfanyabiashara Bw Timothy Muriuki katika hoteli moja jijini Nairobi mwezi uliopita, hakimu mkazi katika mahakama ya Nairobi Bi Miriam Mugure aliambiwa Jumanne.

Kiongozi wa mashtaka Bi Anne Pertet alisema polisi hawakukamilisha uchunguzi wa kesi dhidi ya Bw Sangira Stephen Ochola kwa vile hawakuwa na nambari yake ya simu.

“Polisi walitaka kuitisha orodha ya simu ambazo Bw Ochola alipiga kabla na baada ya kisa hicho. Hawakufanya chochote lakini sasa wameipata watapeleka ombi kwa Safaricom wapewe sajili ya simu alizopiga mshukiwa huyu,” alisema Bi Pertet.

Aliomba kesi hiyo itajwe baada ya wiki mbili ndipo ripoti iwasilishwe ikiwa mshukiwa huyo atafunguliwa shtaka la wizi wa mabavu.

Bi Mugure aliamuru kesi dhidi Bw Ochola litajwe mnamo Juni 4, 2018.

Alipofikishwa kortini wiki iliyopita wakili Cliff Ombeta alipinga mwanahabari huyu akizuiliwa kwa muda wa siku saba kuwezesha polisi kumhoji na kutambuliwa na mlalamishi ambaye aliporwa Sh100,000 na waliomshambulia.

Akiwasilisha ombi la kumzuilia Bw Ochola ,  Koplo Francis Mwita alisema polisi wanachunguza kosa la wizi wa mabavu.

Lakini Mawakili  Ombeta, Nelson Havi , Michael Osundwa , Rodger Sagana  na Harun Ndubi walimweleza hakimu polisi wanataka kumtesa mshukiwa kwa vile walikuwa wamemshtaki Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki Simon Mbugua na washukiwa wengine wawili kwa wizi wa mabavu.