Habari Mseto

Polisi wakana madai kuwa wanahusika na ujambazi

November 7th, 2018 Kusoma ni dakika: 4

NA MOHAMED AHMED

KAMANDA wa Polisi Kaunti ya Mombasa, Bw Johnston Ipara amepinga madai ya wakazi wa mtaa wa Kadzandani kuwa polisi wanahusika na uhalifu eneo hilo.

Badala yake, Bw Ipara alizua maswali kuhusiana na ushahidi wa matukio hayo.

“Nani yuko na thibitisho kuwa kuna afisa ambaye amehusika katika uhalifu huo. Maafisa wetu wanajulikana na kama kuna mtu yeyote ambaye ana ushahidi basi ajitokeze na sisi tutashughulikia hilo,” akasema Bw Ipara.

Wakazi wa Kisauni kaunti ya Mombasa wanaishi kwa hofu kufuatia madai kuwa kuna watu wanaoaminika kuwa maafisa wa polisi wanaohusika katika uhalifu unaoendelea eneo hilo

Katika muda wa wiki mbili zilizopita wakazi wa maeneo bunge ya Nyali na Kisauni wamelalamikia kuvamiwa na kuibiwa na watu hao.

Juma lililopita pekee, takriban matukio sita ya uhalifu yaliripotiwa katika eneo la Kadzandani eneobunge la Nyali.

Imeibuka kuwa afisa wa gereza alikuwa miongoni mwa wahalifu hao.

Mnamo Oktoba 24, afisa huyo alinaswa na wakazi wa eneo la Ziwa la Ng’ombe baada ya kujaribu kumpora mkazi wa hapo.

“Mwenzake aliyekuwa naye alitoroka wakati wa kisa hicho cha saa saba usiku. Alipotaka kuchomwa ndio alijitambulisha kuwa yeye ni afisa wa gereza na maafisa wa kutoka Nyali ambao walikuja kumchukua wakamtambua,” akasema afisa wa masuala ya usalama eneo hilo.

Kuhusiana na ripoti za kuhusika kwa watu wanaojifanya maafisa wa polisi na kutekeleza uhalifu, Bw Ipara alisema kuwa yeyote atakayenaswa atapambana na sheria.

“Na yule ambaye atapatikana anajitambulisha kama afisa na yeye sio afisa basi tukipata ripoti hiyo tutapambana naye. Na kwa afisa ambaye atakuwa akishikilia doria ni lazima ajitambulishe na iwapo hatajitambulisha basi yeye pia ni mhalifu,” akasema Bw Ipara.

Alisema kuwa uchunguzi wa ziada unaendelezwa kuhusiana na visa vya uhalifu katika eneo la Soweto.

Bw Ipara alitoa maombi kwa wakazi kujitokeza na kuripoti visa vinavyodaiwa kutekelezwa maeneo yoyote yale na kuongeza kuwa bila ya visa kuripotiwa inakuwa vigumu kwa maafisa wa usalama kupambana na matukio.

Aidha, baadhi ya wakazi walieleza hofu yao kuhusiana na kuripoti baadhi ya visa hivyo huku wengine wakidai kuwa usalama wao haujahakikishwa.

“Wengine imekuwa ngumu kwetu kujuwa iwapo ni polisi ndio wanahusika katika visa hivi ama ni watu ambao wanajuana na polisi hao na ndio maana kuripoti visa hivi imekuwa ngumu kwetu,” akasema Bw Salim Rajab, mkazi wa Kisauni.

Eneo hilo la Kisauni kwa jumla kwa muda sasa limekumbwa na matukio ya uhalifu ambayo yamewakosesha wakazi usingizi.

Kuna makundi kadha ambayo yametajwa kuibuka eneo hilo na ambayo yanawahangaisha wakazi usiku na mchana.

Makundi hayo pia yametajwa kuhusisha vijana wa umri mdogo na ambaowanahangaisha wakazi bila kujali lolote.

Watu kadha wameuawa kutokana na matukio ya ujambazi, huku baadhi ya washukiwa wa magenge hayo ya vijana pia wakiangamizwa.

Wenye biashara pia wamejitokeza kulalamika jinsi ukosefu wa usalama unaathiri biashara zao, wamiliki wa nyumba wakiwa miongoni mwa walioathiriwa zaidi wakazi wakiamua kuhamia maeneo mengine salama.