Polisi wasaka wazazi waliotupa mtoto aliyezaliwa bila mikono na miguu
MAAFISA wa upelelezi katika Kaunti ya Trans Nzoia wanawasaka wazazi wanaoshukiwa walimtupa mtoto wao mchanga ambaye alizaliwa bila mikono na miguu.
Maafisa wa upelelezi katika Mji wa Kitale Jumanne asubuhi walimuokoa mtoto huyo mchanga asiye na mikono na miguu ambaye alipatikana ametupwa kwenye jaa la taka, huku polisi wakianzisha msako wa kuwasaka wazazi wake.
Mtoto huyo wa kike anayeaminika kuzaliwa siku chache zilizopita alipatikana na wakazi waliokuwa wakipita karibu na jaa asubuhi. Inashukiwa kuwa mtoto aliyezaliwa bila mikono na miguu alitupwa Jumatatu usiku.
Tayari wapelelezi, katika uchunguzi wa awali, wamegundua kuwa mtoto huyo alizaliwa katika hospitali ya eneo hilo, na wazazi walikuwa wamemkataa.
Mtoto huyo alikuwa amefungwa kwa kipande cha kitambaa na kuwekwa kwenye begi alipopatikana.
Wapita njia walisikia sauti hafifu ya mtoto akilia na walipokaribia, walimpata kwenye begi la kubebea mizigo.
Waliarifu chifu wa eneo hilo ambaye alifahamisha maafisa wa polisi waliomuokoa mtoto huyo.
Chifu Charles Namunyu alisema kuwa kutokana na hali yake mtoto huyo anashukiwa kutupwa na wazazi wake usiku au mapema asubuhi.
Kulingana na maafisa wa upelelezi, uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa mtoto huyo alizaliwa katika Hospitali ya Misheni ya St Rafael huko Matisi siku chache zilizopita na alikuwa amekataliwa na wazazi wake.
“Tumegundua kuwa mtoto huyu alikataliwa na wazazi wake na maafisa kutoka Idara ya Watoto ilibidi kuzungumza nao kabla ya mama kukubali kumnyonyesha,” Bw Namunyu alifichua.