Polisi watafuta aliyewasilisha bunduki kanisani akidai ameokoka
NA GITONGA MARETE
POLISI mjini Meru wanamtafuta mwanamume ambaye anasemekana aliwasilisha bunduki kanisani, akidai kwamba ameokoka na dhambi zake kusamehewa.
Jumanne alasiri, polisi walishtuka wakati ambapo Pasta Nathan Kirimi alifika katika kituo cha polisi cha Meru Central akiwa na bunduki ya AK47 na kudai kwamba silaha hiyo iliwasilishwa na mwanamume aliyedai kwamba alikuwa amempokea Yesu kama Bwana na Mwokozi wa maisha yake.
Kamanda wa polisi wa kaunti ndogo ya Imenti Kaskazini Ezekiel Chepkwony alisema wakati Pasta Kirimi wa Jesus Winner Ministries aliingia kwenye kituo na gari akiwa na bunduki hiyo ambayo ilikuwa imefungwa na jaketi na kuwekwa ndani ya gunia, walishtuka sana.
Aliandikisha taarifa ambapo alidai kwamba wakati wa misa Jumapili, kundi la watu ambao walitaka kupeana maisha yao kwa Yesu walipiga magoti mbele yake kama kawaida na akawaombea ukombozi.
“Alisema baada ya misa, mwanamume mmoja alimjia na kusema kwamba alikuwa na ushuhuda, kwamba alitaka kuwasilisha silaha,” akasema Bw Chepkwony kwenye mahojiano na Taifa Leo. Mwanamume huyo aliingia kanisani na kuacha bunduki hiyo mle, alisema.
Afisa huyo wa polisi alisema bunduki hiyo ilikaa kama ilikuwa imefichwa mahali kwa muda mrefu, pengine kuzikwa ardhini kwa sababu ilikuwa na dalili za kumea kutu.
“Hakukuwa na risasi, lakini pasta huyo aliwasilisha maganda 17 ambayo hutumika kwenye mafunzo, au kutishia watu. Lakini la ajabu ni kwamba humu nchini, hatutumii maganda ya AK47,” akasema.