Habari Mseto

Polisi wathibitisha kifo cha Fred Omondi, nduguye Erico

June 15th, 2024 1 min read

NA WINNIE ONYANDO

POLISI wamethibitisha kifo cha Fredrick Odhiambo Omondi, nduguye mcheshi Eric Omondi.

Kulingana na ripoti ya polisi, Fred aliaga dunia baada ya kugongwa na gari Jumamosi asubuhi karibu na kituo cha mafuta cha Caltex katika barabara ya Kangundo.

Kwa mujibu wa taarifa za polisi, ajali hiyo ilihusisha basi la Mitsubishi (namba za usajili KCC 126A) la kampuni ya Forward Travellers Sacco na pikipiki iliyokuwa ikitokea upande mwingine.

“Ajali hiyo ilihusisha basi la Mitsubishi (namba za usajili KCC 126A) lla kampuni ya Forward Sacco, lililokuwa likiendeshwa na Stephen Maina kutoka Kayole, kuelekea CBD, pikipiki iliyombeba mwathiriwa ilikuwa ikitokea upande wa pili. Ajali hiyo ilitokea karibu na Consolidated Bank na Fredrick Odhiambo Omondi aliyekuwa amebebwa na bodaboda alifariki papo hapo,” taarifa ya polisi ilisema.

Taarifa zaidi kutoka kwa polisi zilisema, “Mwathiriwa huyo alipata majeraha makubwa kwenye miguu yote miwili ya kulia na kuvunjika mikono yote miwili. Alikimbizwa katika Hospitali ya Mama Lucy kwa matibabu ila akaaga. Mwili wa marehemu umelazwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha hospitali hiyo ukisubiri kufanyiwa upasuaji.”

Eric Omondi pia alithibitisha kifo cha nduguye kwenye mtandao wake wa kijamii wa Instagram, akisema, “Nenda salama ndugu yangu.”

Familia ya marehemu pia imepokea rambirambi nyingi kutoka kwa watu mashuhuri katika tasnia ya burudani nchini Kenya.

David Mathenge, anayefahamika zaidi kama Nameless, Eunice Wanjiru Njoki almaarufu Mammito, na Daniel “Churchill” Ndambuki ni miongoni mwa wasanii ambao wametuma rambirambi zao kwa familia ya Erico.

Fred pia alikuwa mcheshi na alikuwa kijana mchapa kazi chipukizi katika tasnia hiyo.