Polisi watibua maandamano ya daraja mbovu
NA WYCLIFFE NYABERI
MAAFISA wa polisi wametibua maandamano ya baadhi ya wakazi wa eneobunge la Bobasi, Kaunti ya Kisii, waliokuwa wakilalamikia kutotengenezwa kwa Daraja la Nyamache.
Wakazi hao walirushiwa vitoa machozi walipojaribu kuingia katika makao makuu ya Kaunti Ndogo ya Nyamache, ambapo kuna afisi za utawala za eneo hilo na zile za mbunge Innocent Obiri.
Wakiongozwa na madiwani Michael Motume (Masige Mashariki) na Jacob Bagaka (Masige Magharibi), waandamanaji hao walitaka kuwasilisha stakabadhi muhimu katika afisi za Bw Obiri kumwomba aharakishe ukarabati wa daraja hilo.
Daraja hilo liliporomoka Mei 2023 na wakazi wa eneo hilo wamekuwa wakitaabika kwenye shughuli za uchukuzi.
Pia wamekuwa wakihangaika kufikia afisi za Naibu Kamishina wa Nyamache, makanisa, kufika sokoni
“Watu wetu wameteseka sana. Imekuwa vigumu kuvuka upande mmoja hadi mwingine baada ya daraja hilo kuanguka. Watu wetu wanahangaika kupata hata huduma za serikali kwa sababu ya kivukio hicho.
Tunamtaka mbunge wetu Obiri afanye jitihada daraja hilo litengenezwe. La sivyo, tutazidi kumwekea joto kwani tumechoka sasa,” Bw Motume akasema.
Naye Bw Bagaka alisema watazidi kufanya maandamano kila baada ya wiki mbili kushinikiza uundwaji wa kivukio hicho.
“Tunamtaka mbunge wetu kuwajibika. Ikiwa hatagutuka, tutakusanya sahihi za kumuondoa afisini,” Bw Bagaka alitishia.
Mbunge Obiri katika hafla zake za awali akiwa kwenye eneo wakilishi lake, alisema alikuwa amewasilisha suala la kuporomoka kwa daraja hilo kwa idara husika.
Mbunge huyo aliwataka watu wa Nyamache kuwa na subira akiahidi kuwa kivukio hicho kitatengenezwa.
Kwa muda huo wote ambapo daraja hilo limesalia kuanguka, wakazi wamekuwa wakizunguka mji huo kupata huduma.