Polisi waua bosi wao waliyeshuku ni jambazi
Na BENSON MATHEKA
MAAFISA wa polisi jijini Nairobi, Jumatano usiku walimuua mwenzao wa cheo cha Inspekta katika kisa cha ufyatulianaji wa risasi.
Inspekta Benson Indeche aliyekuwa Naibu Mkuu wa kituo cha polisi cha Riruta, alipigwa risasi na maafisa waliokuwa kwenye doria mtaani Kawangware saa tisa alfajiri akiwahangaisha wahudumu wa bodaboda.
Kulingana na ripoti ya polisi, maafisa hao walipashwa habari na wanabodaboda katika eneo linalofahamika kama Coastal mtaani Kawangware, kwamba kulikuwa na mtu aliyekuwa akiwatisha kwa bastola.
Wahudumu hao waliwafahamisha maafisa hao kwamba, mtu huyo alionekana kuwa mlevi.
“Maafisa wa polisi waliokuwa kwenye doria walienda eneo hilo na kumkabili mtu huyo wakitaka kujua alikuwa nani. Hata hivyo, badala ya kujisalimisha kwao, alichomoa bastola na kufyatulia risasi akamjeruhi afisa mmoja kwenye kiwiko cha mkono. Maafisa hao walijibu kwa kumpiga risasi,” ilisema taarifa ya polisi.
Afisa aliyepigwa risasi alitambuliwa kama Konstebo Kennedy Kimathi na anaendelea kutibiwa katika hospitali ya Nairobi Women.
Inasemekana baada ya kumpiga risasi, walipekua mifuko ya nguo zake na wakagundua alikuwa afisa wa polisi wa cheo cha Inspekta kwa jina Benson Indeche. Ripoti ya polisi ilisema kwamba, alikuwa na bastola aina ya Ceska aliyotumia kumpiga risasi Bw Kimathi.
Baada ya kugundua walikuwa wamempiga risasi mkubwa wao, maafisa hao walimkimbiza katika hospitali ya Nairobi Women, tawi la Adams Arcade ambapo madaktari walipata alikuwa amekufa.
Maafisa hao walieleza kwamba, Indeche alikuwa ametumia risasi saba kutoka bastola yake na haikujulikana iwapo alizifyatua zote wakati wa kisa hicho.
Mwili wa afisa huyo ulipelekwa katika mochari ya Chiromo huku uchunguzi ukianzishwa kubaini jinsi kisa hicho kilitokea.
Katika kisa kingine jijini, maafisa wa polisi waligeuka majambazi na kupora Sh72 milioni kutoka mitambo ya ATM ya benki ya Standard Chartered mtaani Nairobi West.