• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 1:14 PM
Polisi wavunja kambi ya MRC msituni na kunasa silaha

Polisi wavunja kambi ya MRC msituni na kunasa silaha

Na WACHIRA MWANGI

Polisi wameelezea hofu kwamba, kundi la Mombasa Republican Council (MRC) limefufuliwa upya, baada ya kufumania genge la vijana wakipokea mafunzo ya kivita na kujiandaa kwa mashambulizi katika Msitu wa Kaya Jibana eneo la Mulola, Kaunti ya Kilifi.

Afisa Mkuu wa Polisi Kaloleni, Bw Kennedy Osando alisema walipokea habari mnamo Mei 9, kuhusu kikundi cha vijana wapatao 60 ambao walikuwa wamekusanyika msituni humo.

“Tunaamini walikuwa wanajiandaa kutenda uhalifu. Wote walikuwa wamejihami kwa silaha tofauti,yakiwemo mapanga yenye makali. Wengine wao walikuwa bado wananoa makali kwa mapanga yao huku wengine wakicheza densi,” akasema Bw Osando.

Maafisa walipofika katika kambi hiyo haramu ya kivita, waliamuru genge hilo lijisalimishe lakini wakakataa. Katika hali hiyo, ilibidi polisi wafyatue risasi huku wakiwakimbiza vijana hao waliokuwa wakitoroka.

“Walikimbilia mwituni na kuacha mapanga kumi yenye makali. Kutokana na giza lililokuwepo, tuliondoka na kurejea tena alfajiri Ijumaa kisha tukasafisha eneo la uhalifu. Tulichukua baadhi ya silaha zilizokuwepo ikiwemo mapanga, mishale na nyuta kadhaa,” akasema OCPD huyo.

Alisema polisi walikamata vijana wawili na mwanamume mkongwe anayeaminika kuwa mganga wao ambao watafikishwa mahakamani kesho.

“Hawa watu walikuwa wamejiandaa. Walikuwa katika kambi ya mafunzo ya kivita na tayari kutekeleza uhalifu dhidi ya binadamu,” akasema.

Bw Osando aliomba wananchi kupiga ripoti kuhusu mtu yeyote ambaye ataonekana akitafuta matibabu kwa majeraha ya risasi mahali popote kwani inaaminika baadhi ya vijana walitoroka wakiwa na majeraha ya risasi.

Aliomba pia umma kufahamisha polisi ikiwa watasikia kuhusu mazishi ya mtu yeyote bila cheti cha kifo kwani huenda kuna walioangamizwa polisi walipofyatua risasi.

Alionya viongozi, wafuasi na watu wanaoficha wanachama wa MRC kwamba watapatikana hivi karibuni na kuadhibiwa kisheria.

Aliomba wazee wa Kaya wasiruhusu shughuli haramu kuendelezwa katika sehemu wanazosimamia.

You can share this post!

‘Tangatanga’ wazidi kubanwa

Miili yazidi kupatikana mitoni jiji la Nairobi likisafishwa

adminleo