Polisi wazima mikutano ya Kalonzo
Na KITAVI MUTUA
POLISI katika Kaunti ya Tharaka Nithi, jana walimzuia kiongozi wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka kuhutubia mikutano miwili ya hadhara katika miji ya Ndagani na Chuka.
Bw Musyoka ambaye yuko katika ziara ya siku tatu katika eneo la Mlima Kenya Mashariki, alitarajiwa kuwasili katika miji hiyo alasiri katika awamu yake ya pili ya ziara yake ya kukutana na watu.
Waandalizi wa ziara hiyo wakiongozwa na Wakili Kirimi Muturi walikuwa wamemwandikia Afisa Mkuu wa Kituo cha Polisi cha Chuka (OCS) mnamo Februari 10, kuwaarifu polisi na kuomba wadumishe usalama wakati wa mikutano hiyo.
Mkuu huyo wa polisi alijibu kwa kurudisha barua kutoka kwa chama cha Wiper akieleza kwa sentesi moja kuwa mikutano hiyo haikuruhusiwa.
“Mikutano katika kituo cha mabasi mji wa Ndagani na Chuka imekataliwa,” afisa huyoalisema katika jibu fupi akikataa ombi la Wiper.
Kulingana na barua ambayo Taifa Leo iliona, Bw Muturi alikuwa ameeleza kuwa Bw Musyoka na washirika wake wangekutana na wafuasi wao na kuomba usalama kudumishwa ikihitajika.
Kiongozi huyo wa chama cha Wiper ameandamana na waliokuwa Mawaziri Eugene Wamalwa na Peter Munya, Seneta wa Kitui Enoch Wambua na Wabunge kadhaa na madiwani.
Kamanda wa Polisi wa Kaunti ya Tharaka Nithi Zacheas Ng’eno alisema waandalizi wa mikutano hiyo hawakuzingatia sheria na ndiyo sababu aliamua kufutilia mbali mikutano hiyo.
Bw Ng’eno alisema barua ilipokelewa na mkuu wa kituo cha polisi katika eneo husika mnamo Jumapili kinyume na masharti ya kisheria ya angalau siku tatu kabla ya tarehe ya mkutano.
“Leo ni Februari 12, barua iliandikwa tarehe 10 na ombi kuwasilishwa Februari 11. Sivyo inavyopaswa kuwa,” alisema Kamanda wa Polisi wa Kaunti hiyo. Alionya kuwa kuwa kikosi cha Wiper hakitaruhusiwa kuhutubia mikutano yao ya hadhara iliyopangwa.
Hata hivyo, waandalizi waliapa kuendelea na mikutano hiyo wakisema walitimiza masharti ya sheria na ni jukumu la Kikatiba la Huduma ya Kitaifa ya Polisi kuwapa usalama wa kutosha.
Bw Wambua alisema kwa kutaka kuharamisha mikutano halali wa Wakenya, polisi walikuwa wakitumiwa na serikali ya Kenya Kwanza kukandamiza uhuru wa kimsingi wa kujumuika, ambao umebainishwa katika Katiba.
“Hatutaruhusu mtu yeyote kutunyang’anya haki zetu za kimsingi na uhuru. Tutaendelea na mikutano jinsi ilivyopangwa kwa sababu hatujafanya kosa lolote,” alisema Seneta Wambua.
Gavana wa Makueni Mutula Kilonzo Junior alipuuzilia mbali jaribio la polisi kumzuia kiongozi wa chama chake kuhutubia mikutano hiyo miwili akisema ni kinyume cha katiba na halina msingi wowote wa kisheria.
Gavana Kilonzo alisema kinachohitajika ni ilani kuhusu mkutano kwa polisi.
“Uhuru wa kukutana hauwezi kuzimwa isipokuwa palipo na tishio kwa usalama au kwa amani. Hali ikiwa hivyo, polisi wanafaa kueleza tishio lilipo kwa amani au usalama,” alisema.
Kaunti ya Tharaka Nithi ni nyumbani kwa Waziri wa Usalama wa ndani kituo cha mabasi cha Chuka waandalizi walikuwa wameweka Kithure Kindiki.