Habari Mseto

Pombe: Shughuli zasimama sokoni Muthurwa washukiwa wakikamatwa

March 12th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

NA SAMMY KIMATU

WASHUKIWA 56 wamekamatwa wakati wa msako dhidi ya pombe haramu uliofanyika Muthurwa katika Kaunti ya Nairobi.

Operesheni hiyo iliongozwa na Naibu Kamishna wa Kaunti ndogo ya Starehe John Kisang akishirikiana na Kamanda wa Polisi wa Central Doris Mugambi miongoni mwa maafisa wengine katika idara mseto za serikali.

“Operesheni yetu ilikuwa ni ya kupambana kumaliza vileo vilivyoharamishwa na serikali ili kuokoa wananchi wasiangamizwe na pombe,” Bw Kisang akawaambia wanahabari.

Aliongeza sababu nyingine ni kwamba biashara ya aina hiyo inainyima serikali mapato kupitia njia za mkato.

Bi Mugambi alisema ni jukumu la polisi kulinda wananchi na mali yao huku wakitekeleza wajibu wao kama maafisa kikatiba na kuhakikisha sheria za Kenya zimefuatwa.

Baadhi ya pombe iliyonaswa ni pamoja na lita 2,400 za miti ni dawa, lita 200 za busaa, kilo 20 za mbegu za bangi, lita mbili za chang’aa, mitungi 14 ya lita 200, kreti 88 za pombe inayotengenezwa hivihivi, katoni mbili za pombe ya makali, kilo 89 za sukari guru na katoni moja ya hamira (chachu).

Shughuli zilisimama kwa muda katika eneo lililokuwa na msako huku wananchi waliokuwa katika soko la Muthurwa wakifurika kila mmoja apate nafasi ya kushuhudia.