Habari Mseto

PrideInn yawafaa wafungwa wanawake Shimo La Tewa kwa kuwapa malazi na sodo

May 23rd, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na WINNIE ATIENO

WANAWAKE wafungwa katika gereza la Shimo La Tewa wamepata afueni baada ya hoteli ya kifahari ya PrideInn kuwapa magodoro, mashuka na sodo.

Aidha wanawake hao ambao wamekuwa wakihangaika kufuatia mvua kubwa inayoendelea kunyesha sehemu za Pwani wamepata afueni baada ya wasimamizi wa hoteli hiyo kuwafadhili kwa vifaa hivyo muhimu.

Kulingana na wasimamizi wa hoteli hiyo, magodoro, mashuka na sodo zitatumiwa na wanawake 100 kwenye gereza hilo waweze kujikidhi na kujisitiri baridi kali Mombasa.

Afisa msimamizi wa gereza hilo huko Shanzu Bi Josephine Mutuku ameshukuru hoteli hiyo kwa ufadhili huo akisisitiza wafungwa wenye watoto watanufaika pakubwa na magodoro, mashuka na sodo hizo.

“Haya ni makao yao wanapoendelea kutumikia vifungu vyao huku wakipata mafunzo kadha wa kadha ambayo watatumia kujimudu watakapotoka gerezani na kujumuika na umma. Ufadhili huu utasaidia sana kudumisha usafi gerezani hususan sehemu ya wafungwa wenye watoto,” akasema Bi Mutuku.

Amesema mvua kubwa inayoendelea kunyesha sehemu kadha wa kadha nchini ikiwemo Mombasa imesababisha changamoto katika kudumisha mazingira safi.

Wasimamizi wa hoteli, pia wamewapa nasaha wafungwa hao na kuwapa mafunzo ya kudumisha usafi na kuosha mikono ili wajilinde dhidi ya virusi vya corona.

“Tuliamua kuja kuwasaidia sababu mara nyingi, wafungwa huwa wamesahaulika katika jamii hususan wakati huu ambapo wanahitaji msaada. Wanawake walio gerezani wanahitaji msaada unaohusu maswala ya afya au lishe bora, magodoro, sodo, miongoni mwa bidhaa zingine za uzazi,” akasema Bi Ann Peggy, mkurugenzi mkuu wa PrideInn Paradise Beach.

Akaongeza kwamba mashuka hayo yatawasaidia wakazi kujikimu na wana wao kutokana na baridi na magonjwa yanayotokana na hali hiyo ya hewa.

Mkurugenzi mkuu wa hoteli za PrideInn eneo la Pwani Bw Victor Shitakah, amewasihi Wakenya wajitokeze kuwasaidia wafungwa akisisitiza wanakabiliwa na changamoto tele.