Habari Mseto

Profesa akanusha kumshambulia mwenzake

November 1st, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na BENSON MATHEKA

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Katoliki jijini Nairobi, Jumatano alishtakiwa kwa kumshambulia mwenzake ndani ya chuo hicho na kumjeruhi.

Profesa Samuel Ndiritu Nyaguaya ambaye anasimamisha huduma za wanafunzi katika chuo hicho, alifika katika mahakama ya Kibera na kukanusha kwamba alimdhuru Profesa Rosa Ko.

Mahakama iliambiwa kwamba Profesa Ndiritu alitenda kosa hilo Oktoba 3 mwaka huu akiwa katika chuo hicho kilichoko Karen jijini Nairobi.

Kesi hiyo ilikuwa imeahirishwa mara tatu kwa sababu mshtakiwa hakuwa akifika kortini alivyoagizwa na polisi waliomkamata malalamishi yalipowasilishwa.

Jana, Profesa Ndiritu alieleza Hakimu Mkuu Mkazi Faith Mutuku kwamba hakuwa amejificha ilivyodaiwa na mlalamishi mbali alikuwa nje ya Nairobi kwa shughuli za kikazi.

“Sikuwa nimejificha, inajulikana wazi nilikuwa Nyeri kwa shughuli za kikazi,” alisema.

Aidha, alikanusha kwamba amekuwa akiwachochea wahadhiri wa chuo hicho dhidi ya mlalamishi ambaye ni raia wa Amerika.

Kiongozi wa mashtaka Nancy Kerubo alifahamisha mahakama kwamba mlalamishi na mshtakiwa ni wafanyakazi wa chuo hicho na akaomba agizo la kumzuia Profesa Ndiritu dhidi ya vitendo vya uchochezi.

“Ninashangaa kusikia eti ninachochea wahadhiri ambao ni maprofesa. Ni vigumu, maprofesa hawawezi kuchochewa. Ni wasomi wanaofanya uamuzi wao wenyewe na madai ya mlalamishi hayana msingi,” alisema Profesa Ndiritu kupitia wakili wake.

Bi Mutuku alimwachilia kwa dhamana ya Sh50,000 na mdhamini wa kiasi sawa au Sh30, 000 pesa taslimu hadi Februari 14 2019 kesi itaposikilizwa.

Alimuagiza kutohusika na vitendo vyovyote vya uchochezi dhidi ya mlalamishi.

“ Unaonywa wewe binafsi au maajenti wako kutohusika na vitendo vya uchochezi. Epuka hatua zinazoweza kuathiri kwa vyovyote kesi iliyoko kortini,” hakimu aliagiza.