Habari Mseto

Programu ya i-Cut yasaidia wasichana Wakenya kutambulika Sakharov

October 28th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na MAGDALENE WANJA

WANAFUNZI watano kutoka Kenya ni miongoni mwa watu bora katika Tuzo ya Sakharov ya mwaka 2019.

Wanafunzi hao ni Ivy Akinyi, Purity Achieng’, Synthia Otieno, Stacy Adhiambo, na Macrine Atieno.

Wanafunzi hao kutoka shule ya upili ya wasichana ya Kisumu Girls, walichaguliwa kutokana na ubunifu wao katika vita dhidi ya ukeketaji wa wanawake kwa kutumia teknolojia ya programu ya simu (mobile app).

Uchaguzi huo ulifanyika siku ya Jumatano.

“Washindi watatuzwa katika bunge la Strasbourg mnamo Jumatano, Desemba 18, 2019,” ilisema taarifa kutoka kwa afisa wa mawasiliano katika ofisi ya Ujumbe wa Muungano wa Ulaya wenye shughuli zake nchini Kenya.

Programu hiyo kwa jina i-Cut itawapa wanawake nafasi ya kuripoti visa vya ukeketaji ambapo wanaweza ‘kuitisha usaidizi’, ‘kunusuriwa au kuokolewa’, ‘kuripoti’, ‘kupata taarifa kuhusu ukeketaji’ na ‘kutoa mchango na majibu’.

Kulingana na waandalizi wa tuzo hiyo, ubunifu huo una maana sana kwani utachangia katika kupunguza visa vya wasichana wanaoacha masomo yao na kujipata katika hali ambayo uhai wao unakuwa hatarini.

“Ukeketaji una madhara makubwa ya kiafya na unaweza kusababisha kifo. Mbali na hayo, unawafanya wasichana kukatiza elimu yao ya shuleni na kuwanyima nafasi ya kuwa na maisha bora,” ilisema taarifa hiyo.

Teknolojia hii ni njia mojawapo ya kuwapa wasichana nafasi na uwezo wa kuamua jinsi ambavyo wanaweza kuendesha maisha yao.

“Hata hivyo, tumaini letu ni zaidi ya ushindi wa tuzo hii kwani cha muhimu sana ni kutambua kitendo hiki cha kujitolea kuwaokoa wasichana kutoka kwa tamaduni hii potovu.”

Programu ya i-Cut imewahi kuwashindia tuzo kwa jina ‘Prestigious African of the Year Award’ ya Mwaka 2018.