Punguzeni mbio: UDA sasa yaita madiwani kujaribu kuwashawishi wamwache Gavana Mutai
CHAMA cha United Democratic Alliance (UDA), kimechukua hatua kujaribu kumuokoa Gavana wa Kericho, Bw Erick Mutai (pichani) asitimuliwe ofisini kwa kuwaita madiwani wote 38 wa Bunge la Kaunti kwa mkutano kuhusu mzozo huo.
Katika barua iliyoandikwa Septemba 30, 2024, Katibu Mkuu wa UDA, Bw Hassan Omar, aliitisha mkutano huo jana katika juhudi za kuzima msukosuko wa kisiasa na uwezekano wa kutimuliwa kwa Gavana Mutai.
“Chama kimekuwa kikifuatilia kwa makini matukio katika Kaunti ya Kericho na haswa suala linalohusu kuondolewa ofisini kwa gavana. Ni maoni yetu kwamba uwiano na utaratibu mzuri wa kaunti ni muhimu ili kutuwezesha kutimiza ahadi zetu za uchaguzi,” Bw Omar alisema, akisisitiza haja ya uwiano na utulivu katika kaunti.
Wakati huo huo, serikali imeagiza uchunguzi kufanywa katika shule mbili za Trans Nzoia zilizofungwa kuhusiana na madai ya matumizi mabaya ya fedha baada ya wanafunzi kuandamana wiki jana.
Shule ya Upili ya Wasichana ya Mtakatifu Monica na Shule ya Sekondari ya Friends Namanjalala zilifungwa kwa muda usiojulikana baada ya wazazi na wanafunzi kulalamikia usimamizi mbovu.
Kamishna wa Kaunti Bw Gideon Oyagi, alifichua kuwa Wizara ya Elimu imeanzisha uchunguzi wa kina kuhusiana na madai ya usalama wa wanafunzi shuleni na lishe duni kwa wanafunzi yaliyoibuliwa na wazazi.
“Tutafanya uchunguzi kuhakikisha tunachunguza kwa kina suala hili na kupata ripoti itakayotusaidia kuchukua hatua,” alisema Bw Oyagi.