• Nairobi
  • Last Updated May 8th, 2024 5:03 AM
Purukushani walimu wakuu wakimrushia chupa Ndolo kupinga ada

Purukushani walimu wakuu wakimrushia chupa Ndolo kupinga ada

Na WINNIE ATIENO

WALIMU wakuu wa shule za msingi Jumatatu walivurugana kwenye kongamano la kitaifa mjini Mombasa wakizozania ada ya Sh500.

Wakiwa wamepandwa na mori, walimtaka mwenyekiti wao Bw Shem Ndolo ajiuzulu, wakimshtumu kwa kutoonyesha manufaa ya wao kuchanga Sh500 kila mwezi.

Aidha, walisema hawakubaliani na msimamo wa mwenyekiti huyo, kwamba anapinga mgomo uliotangazwa na chama cha kutetea walimu cha Knut, pamoja na kuwa anaunga mkono uhamisho wa walimu unaotekelezwa na tume ya kuajiri walimu (TSC).

Zaidi ya walimu 200 walimshambulia Bw Ndolo na kumtaka ajiuzulu kama hayuko tayari kupunguza ada ambayo awali ilikuwa Sh100 kabla ya kupandishwa hadi Sh500.

“Inashangaza sana sababu zao kupinga nyongeza hiyo ilhali ni wao waliopitisha kwa kauli moja mwaka jana. Ndio maana nashuku wametumwa kuzua taharuki na ghasia kwenye mkutano huu ambao umekuwa na utulivu kwa miaka na mikaka” akasisitzia Bw Ndolo.

Alimwagiwa maji na chupa za maji kurushwa kwenye jukwaa ambapo wakuu wa chama hicho walikuwa wameketi na ikabidi atoroshwe.

Walimu hao wakuu walimkashifu kwa kuwapuuza na kutaja malalamishi yao kuwa ‘upuzi mtupu’.

Bw Ndolo aliomba msamaha kwa kutamka neno upuzi lakini walimu walikataa kumsamehe na kutishia kumng’atua malakani.

“Usitutoze ada hiyo kijumla, kuna walimu wenye wanafunzi katika sehemu kame na wale walioko maeneo ambapo wanafunzi wanaofunzwa ni wa kutoka familia bwenyenye, tunataka muungano uangalie maslahi ya walimu wanaofunza sehemu kame,” akasema Bw Joseph Njeru mwalimu mkuu kutoka Nakuru.

Zaidi ya walimu 10,000 wamekusanyika katika ukumbi wa Sheikh Zayed kwenye warsha yao kujadili maswala yanayowakabili hususan mgomo unaonukia na kuhamishwa kwa walimu kutoka kaunti wanakotoka hadi sehemu zingine nchini ili kuleta uwiano.

Baada ya tukio hilo, mkurugenzi wa elimu ya msingi eneo la Pwani, Bw Abdi Habat na mshirikishi wa eneo hilo, Bw Bernard Leparmarai waliwafokea walimu hao na kuonya kuwa waliozua fujo wataadhibiwa.

“Tutakabiliana na baadhi ya watu hapa, sheria itachukua mkondo wake baada ya Rais kuufungua na kwenda zake, hatutajadili swala la nidhamu ni sharti muwe na adabu na mutii sheria. Kile kisa kilichofanyika ni cha aibu kubwa sana na kisitendeke tena,” Bw Habat akawaonya.

Alisema Rais anafaa kuheshimiwa kw amujib wa katiba.

“Kama mna tofauti zenu, kuna njia nyingi ya kuleta mpatanisho lakini hamuwezi kunialika nyumbani kwake alau unaanza kupigana na mke wako mbele yangu,” akasema kwa kinaya.

  • Tags

You can share this post!

‘Hekima’ ya Waititu kusongesha mito yashtua...

Mkahawa wapiga marufuku sahani, chupa na vijiko vya plastiki

adminleo