Habari Mseto

Pwani kuenda kortini

July 27th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

CHARLES WASONGA na CHARLES LWANGA

VIONGOZI wa Pwani wametisha kuenda kortini kuzuia utekelezwaji wa mfumo mpya wa ugavi wa fedha baini ya kaunti endapo utapitishwa katika seneti Jumanne.

Kwenye taarifa ilitolewa Jumatatu na afisa wa sekritarieti ya Jumuiya ya Kaunti za Pwani (JKP) Emmanuel Nzai, viongozi hao walishikilia kuwa kaunti sita za eneo hili zingali zinapinga mfumo huo licha ya kuungwa mkono na kiongozi wa ODM Raila Odinga na Rais Uhuru Kenyatta.

“Hatuwezi kuunga mkono mfumo huu ambao utasababisha kaunti sita za Pwani kupokonywa jumla ya Sh7 bilioni katika mwaka huu wa kifedha wa 2020/2021 ikilinganishwa na mgao wa mwaka wa kifedha uliopita wa 2019/2020,” akasema Bw Nzai.

Mfumo huo uliotayarishwa na Tume ya Ugavi wa Mapato (CRA) Sh316.5 bilioni zilizotengewa serikali za kaunti katika bajeti ya mwaka huu unaupa uzito mkubwa kigezo cha idadi ya watu.

Hii ina maana kuwa kaunti zenye idadi kubwa ya watu, kulingana na matokeo ya shughuli ya kitaifa ya kuhesabu (Sensa) iliyoendeshwa mwaka 2019, zitapata mgao mkubwa wa fedha ikilinganishwa na mgao wao wa mwaka huo.

Na jumla ya kaunti 18 kutoka Pwani, Kaskazini Mashariki, na maeneo ya jamii za wafugaji zitapoteza jumla ya Sh17 bilioni.

Kwa mfano, katika eneo hili, kaunti za Kilifi na Kwale zitapoteza Sh1.2 bilioni na 1.1 bilioni, mtawalia ikiwa mfumo huo utapitishwa katika seneti mnamo Jumanne. Na kaunti kama Mombasa itapoteza takriban Sh670 milioni.

Kwenye taarifa Jumatatu, kiongozi wa ODM Raila Odinga amewataka maseneta kupitisha mfumo huo akiunga mkono ugavi wa fedha unaoipa idadi ya watu uzito.

Wiki jana, Rais Kenyatta aliwataka wabunge kupitisha mfumo huo akisema utahakikisha haki inatendewa kaunti zenye idadi ya juu ya watu.