• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 12:11 PM
Radi yalipua simu na kuua mama akilala nyumbani

Radi yalipua simu na kuua mama akilala nyumbani

Na WAANDISHI WETU

MWANAMKE wa umri wa miaka 45 alifariki papo hapo baada ya simu yake kulipuka wakati radi ilipotokea ghafla katika kijiji cha Kadibuoro, Rangwe katika Kaunti ya Homa Bay.

Mwanamke huyo aliyetambuliwa kama Mary Akinyi, alifariki papo hapo huku mumewe Patrick Yala wa miaka 50 akinusurika.

Mkasa huo ulitokea Jumapili usiku, baada ya nyumba yao kupigwa na radi.

Kulingana na kakake Bw Yala, Nathaniel Ochieng, mwili wa marehemu ulichomeka kabisa baada ya mlipuko huo.

Bw Ochieng alisema kuwa simu hiyo ililipuka baada ya radi kupiga chombo cha kunasa kawi ya miale ya jua (sola) ambayo ilikuwa inatumiwa kuchaji simu wakati huo wawili hao wakiwa wamelala.

Vifaa vingine vya kielektronini pia viliharibiwa kwenye kisa hicho.

Bw Yala alikimbizwa katika Zahanati ya Ndilu kupokea matibabu akiwa amepoteza fahamu.

Msimamizi mkuu wa zahanati hiyo, Bw Dancun Ngich, alisema Bw Yala alipoteza fahamu kwa mshtuko kutokana na mkasa huo.

Alisema kuwa mwathiriwa alikuwa akitapika damu, jambo lililofanya hali yake kuwa mahututi.

Kwingineko, mechi ya kandanda iligeuka kuwa mkasa katika wadi ya Nangina, eneobunge la Funyula, Kauti ya Busia, baada ya radi kumuua mtu mmoja na kuwajeruhi wengine sita.

Marehemu alitambuliwa kama Allan Mbote aliyekuwa akisherehekea ushindi wa timu ya Red Sharks, aliyokuwa akiishabikia.

Timu hiyo ilikuwa ikicheza dhidi ya Reybentos, kuwania Kombe la Wadi ya Nang’ina katika Shule ya Msingi ya Luchululo.

Marehemu pia alikuwa mwanafunzi wa mwaka wa pili katika Chuo Kikuu cha Kenyatta.

Mkuu wa Polisi katika eneo la Funyula Mary Kiarie, alisema kuwa watu watatu miongoni mwa waliojeruhiwa wanaendelea kupokea matibabu katika Hospitali ya Misheni ya Nangina. Wengine watatu walitibiwa na kuruhusiwa kwenda nyumbani.

Kisa hicho kinatokea siku moja tu baada ya radi kuwaua watu watatu katika kijiji cha Kakapel, Kaunti Ndogo ya Teso Kaskazini.

You can share this post!

Ushirikiano wa Kalonzo na Uhuru hauwasaidii Wakamba –...

UFISADI: Raila awakosoa wandani wa Ruto

adminleo