Raha kijijini chifu aliyetupwa jela miaka 11 kurejeshwa kazini
Na STEPHEN ODUOR
WAKAZI wa eneo la Haroresa, kaunti ya Tana River walijawa na furaha na kushangilia, aliyekuwa chifu wa eneo hilo aliporudishwa kazini rasmi baada ya miaka 11.
Omar Mohammed Ibrahim alikuwa amefutwa kazi baada ya vita vya kijamii vya 2007, akidaiwa kuchochea jamii hizo mbili.
Kesi yake ilichukua mkondo mkali pale idara ya usalama ilipomsimamisva kazi na kumshtaki kwa madai ya uchochezi.
Ni kesi ambayo ataishi kuikumbuka, kwani imemgharimu vikali kiasi cha kumwacha masikini.
Kukosekana kwa huduma zake katika eneo hilo la Haroresa kumezua changamoto tele, huku wakazi wakikosa mwakilishi wa serikali kwa zaidi ya miaka 10.
Wakazi hao kwa zaidi ya miaka mitano wamekuwa wakiwashurutisha viongozi kuingilia kati suala la chifu huyo, huku wakidai asamehewe na kurudishwa kazini kwani aliwafaa sana katika enzi za utawala wake.
Viongozi kadha akiwemo Mbunge wa Galole, Bw Said Hiribae walifuatilia suala hilo, na baada ya miaka 11, mahakama ya juu mjini Malindi ilimpata bila hatia na kuamuru arudishwe kazini mara moja.
Katika hafla hiyo ya kurudishwa mamlakani iliyohudhuriwa na naibu Kamishna wa kaunti, Bw Michael Kioni Bw Ibrahim aliahidi kutekeleza kazi zake bila mapendeleo, huku akiwahimiza wakazi kuisaidia serikali katika kuleta amani Tana River .
“Tuko na kizungumkuti kinachotukabili, na dawa yake ni moja tu, tushirikiane kama jamii, wale wanaokuja kuvuruga amani yetu sio jamaa zetu, tuje pamoja ili tumalize ughaidi, “alisema.
Naibu Kamishna wa kaunti Bw Michael Kioni pia alimhimita chifu huyo kulivalia njuga swala la mwanadada muitaliano Sylvia Romano, uku akimpa jukumu la kufanya ujasusi tosha kubaini alikoficjwa mwanadada huyo.
Bw Ibrahim amekuwa akihudumu kama mzee wa kijiji tangu kusimamishwa kazi, ila hakuruhusiwa kusafiri mbali pasi na kuwajulisha polisi.