Habari Mseto

Raha ya wakulima mswada wa chai ukipita bungeni

December 3rd, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na CHARLES WASONGA

WAKULIMA wa majani chai wana matumaini ya kufaidika pakubwa kutokana na Mswada wa Chai, 2018, uliopitishwa katika Bunge la Kitaifa mnamo Jumanne usiku.

Mswada huo umepokonya Shirika la Ustawi wa Majani Chai nchini (KTDA) mamlaka na udhibiti wa mabilioni ya fedha za wakulima.

Ulipitishwa bila kufanyiwa marekebisho makubwa, ishara kwamba Bunge la Seneti litauidhinisha kwa urahisi kabla ya kuwasilishwa kwa Rais Uhuru Kenyatta autie sahihi ili kuwa rasmi sheria.

Kulingana na mswada huo uliofadhiliwa na Seneta wa Kericho Aaron Cheruiyot, fedha kutokana na mauzo ya zao hilo sasa hazitapelekwa kwa akaunti ya KTDA bali katika akaunti ya viwanda vya majani chai.

“Wakulima watapewa asilimia 50 ya mauzo ya zao lao mnadani, baada ya fedha hizo kupokewa katika akaunti za viwanda; kisha nusu iliyosalia ya fedha hizo watazipokea mwisho wa mwaka,” mswada huo unasema.

Isitoshe, viwanda vya majani chai vitatakiwa kuwapa wakulima katika maeneo yao nusu ya mauzo yote ya zao hilo kila mwezi.

Malipo hayo yote – kutoka kwa mabroka, wanunuzi na madalali wa mnada – katika siku 14 baada ya mauzo; tofauti na hali ilivyo sasa ambapo KTDA huchelewesha fedha hizo kwa hadi mwaka mmoja, huku ikiwatoza ada ya juu ya usimamizi.

Kulingana na Waziri wa Kilimo Peter Munya, KTDA huwatoza wakulima Sh2 bilioni kila mwaka kama ada ya usimamizi.

Hii ina maana kuwa bonasi ambayo wakulima hupokea kila mwaka itaongezeka kuliko mwaka jana ambapo wengi walizoa Sh28 kwa kilo pekee.

Mswada huo unapendekeza kubuniwa kwa Halmashauri ya Kusimama Sekta ya Majani Chai nchini (Tea Regulatory Authority of Kenya) itakayoandaa kanuni za ustawishaji wa zao hilo, uuzaji katika mnada na uuzaji katika masoko ya ng’ambo.

Baadhi ya kanuni hizo za TRAK zilizinduliwa mwaka jana na Waziri wa Kilimo Peter Munya.

Asasi hiyo pia itatwaa majukumu mengine ya KTDA ambayo wakulima wameilaumu kwa usimamizi mbovu uliosababisha kupungua kwa faida yao.

TRAK, ambayo itachukua mahala pa Bodi ya Chai nchini (TBK), itashirikisha serikali za kaunti katika uendeshaji wa sekta hiyo – ambayo huiletea Kenya Sh140 bilioni, kwa wastani, kila mwaka.

Kwa mujibu wa mswada huo, serikali za kaunti ambako majani chai hukuzwa zitasimamia masuala kama: ustawishaji wa majani chai, juhudi za kukabiliana na maradhi yanayokumba mmea huo, masoko, vyama vya ushirika na utunzi wa rotuba ya udongo na uhifadhi wa maji.

Bodi ya usimamizi ya TRAK itaongozwa na mwenyekiti atakayeteuliwa na Rais, kwa ushauri wa Waziri wa Kilimo.

Pia itakuwa na wawakilishi watakaoteuliwa na Baraza la Magavana (CoG) kutoka kaunti saba ambazo hukuza majani chai kwa wingi.

“Wanachama wengine wa bodi ya TRAK watajumuisha watu walioteuliwa na vyama vya wakulima wa majani chai na Afisa Mkuu Mtendaji (CEO) wa halmashauri hiyo,” yaeleza kipengele cha 10 cha mswada huo.

Fauka ya hayo, Mswada unaipa TRAK mamlaka ya usimamizi wa masuala yote katika sekta ya chai; kushirikisha shughuli za watu binafsi na mashirika; na kuwezesha wadau wote katika sekta kunufaika na rasilimali zote za sekta.

Jana, wabunge waliochangia mjadala kuhusu mswada huo walielezea matumaini yao kwamba utasuluhisha changamoto ambazo zimekuwa zikizonga sekta ya chai na kusababisha hasara kwa wakulima.

“Mswada huu utaleta manufaa makubwa kwa wakulima wa majani chai hata kuliko marekebisho ya Katiba kupitia BBI, kwa sababu utawaondoa kutoka utumwa na unyanyasaji wa KTDA” akasisitiza Mbunge Maalum Bi Cecily Mbarire.

Wengine waliouchangamkia mswada huo ni Rigathi Gachagua (Mathira), Ndindi Nyoro (Kiharu), Japheth Mutai (Bureti), Godffrey Osotsi (Mbunge Maalum) miongoni mwa wawakilishi wengine.

Mswada huo umekuwa ukichambuliwa na Kamati ya Bunge kuhusu Kilimo, inayoongozwa na Mbunge wa Moiben Silas Tiren.