Habari Mseto

Raia wa Chad akana kumlaghai Mungatana Sh76 milioni

October 16th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Na RICHARD MUNGUTI

RAIA wa Chad Jumanne alishtakiwa kwa kumlaghai aliyekuwa  waziri msaidizi Bw Danson Mungatana Sh76 milioni akidai atamwekezea katika biashara ya mafuta miaka saba iliyopita..

Bali na kumlaghai Bw Mungatana, Bw Abdoulaye Tamba Kouro alifunguliwa shtaka la kupatikana na pesa za kigeni feki sawa na Sh960,120,000 mtaani Westlands, Nairobi.

Kwa jumla Bw Kouro alikabiliwa na mashtaka manne dhidi yake ya ughushi wa dola za Kimarekani na Euro za Ulaya pamoja na kuwalaghai Mabw Muungatana na Bw Makau Muteke mamilioni ya pesa.

Mshtakiwa alikana mbele ya hakimu mkuu mahakama ya Milimani Bw Francis Andayi  kuwa alimtapeli mwanasiasa huyu ambaye pia ni wakili katika eneo la Hurligham, kaunti ya Nairobi dola za Marekani $1,000,000 zinazokisiwa sawa na Sh76milioni.

Alikana alipokea pesa hizo kutoka kwa Bw Mungatana kwa njia ya udanganyifu kati ya Aprili 20, 2011 na 29, 2013.

Kiongozi wa mashtaka Bi Kajuju Kirimi alimweleza hakimu kuwa Bw Kouro, mwenye umri wa miaka 50 , alimwambia waziri huyo kuwa angemwekezea pesa hizo katika biashara ya mafuta, jambo alilojua ni uwongo.

Raia huyo wa Chad pia alishtakiwa kumlaghai Bw Makau Muteke Dola za Marekani 6,796 (Sh0.7 milioni) akimdanganya atamwekezea katika biashara ambayo Polisi hawakusema katika cheti cha mashtaka.

Mshtakiwa alikana kuwa mnamo Oktoba 1, 2018 katika eneo la Westlands alipatikana akiwa na Dola za Marekani 54,000 za noti za 100 na  sarafu za Euro 19,000 za noti za 100 na Euro nyingine 3,400 za noti za 500.

Thamani ya pesa hizo feki ambazo mshtakiwa alikutwa nazo ni sawa na Sh960,120,000.

Mahakama ilifahamishwa mshtakiwa alikabiliwa na shtaka la pili la kughushi pesa hizo kwa lengo la kuwatapeli wananchi.

Mshtakiwa aliomba aachiliwe kwa dhamana  afanye kesi akiwa nje. Bi Kirimi hakupinga mshtakiwa akiachiliwa kwa dhamana.

Wakili aliyewakilisha walalamishi katika kesi hiyo aliomba mahakama isimwachilie mshtakiwa kwa dhamana kwa vile ni raia wa kigeni.

“Mshtakiwa hawezi kunyimwa dhamana kwa vile ni raia wa kigeni. Katiba inakubalia kila mshtakiwa anayefikishwa mahakamani kuachiliwa kwa dhamana  isipokuwa kuwe na sababu maalum,” Bw Andayi alimweleza wakili huyo.

Hakimu huyo alimwachilia mshtakiwa kwa dhamana ya pesa tasilimu Sh3 milioni.

Akishindwa kupata milioni hizo tatu mahakama ilimweleza awasilishe  hati ya umiliki  shamba lililo na thamani ya shilingi milioni tano au logibuk ya gari iliyo na thamani hiyo.

Zaidi ya hayo mshtakiwa aliamriwa amfikishe mahakamani raia wa Kenya atakayeapa kwa korti kuwa “ kila wakati mshtakiwa atahitajika kufika kortini atahakikisha amefika.”

Bw Andayi aliorodhesha kesi hiyo kusikizwa mnamo Novemba 29, 2018.