Habari Mseto

Raia wa China ashtakiwa kuiba viatu vya mitumba vya Sh3 milioni

July 6th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na RICHARD MUNGUTI

RAIA wa China anayefanya biashara nchini Kenya alishtakiwa Ijumaa kwa kuiba viatu vya mitumba vyenye thamani ya Sh3 milioni.

Li Bingpeng, alikanusha mashtaka mawili aliposhtakiwa mbele ya hakimu mkazi Bi Muthoni Nzibe.

Mahakama ilifahamishwa viatu hivi vya mitumba ndivyo vinavyouzwa katika soko la Gikomba, Kaunti ya Nairobi.

Bingpeng alishtakiwa kwamba Desemba 9, 2018, katika Inland Container Depot jijini Nairobi katika barabara ya Nairobi-Mombasa aliiba kontena ya viatu kuukuu ambapo thamani yake ni Sh3 milioni.

Bi Nzibe alifahamishwa na kiongozi wa mashtaka kwamba viatu hivyo vilikuwa mali ya Bw Peter Gichini Macharia.

Shtaka la pili dhidi ya Bingpeng lilikuwa kwamba mnamo Novemba 8, 2018, katika hoteli ya Eastlands Hotel iliyoko barabara ya Ngong akishirikiana na watu wengine ambao hawakufikishwa kortini, walifanya njama za kuwapora Mabw Stephen Jimmy Mwangangi na Peter Gichini Macharia kiasi cha dola za Kimarekani (USD) 14,831 (Sh1,483,100) wakidai watawauzia viatu kuukuu vyenye thamani ya Sh3 milioni.

Mahakama ilifahamishwa Mchina huyu aliwadanganya Bw Mwangangi na Macharia watawapa nakala za kuingiza viatu hivyo.

“Mlijua mnawadanganya Mabw Mwangangi na Macharia eti mngewauzia viatu hivyo na kuwapa nakala za kuigiza viatu hivyo nchini. Ni kweli Bingpeng?” aliuliza Bi Nzibe.

“Sio ukweli,” Bingpeng alijibu kupitia kwa mkalimani.

Mshtakiwa aliomba aachiliwe kwa dhamana na upande wa mashtaka haukupinga.

Bi Nzibe aliamuru Bingpeng alipe dhamana ya Sh800,000 pesa taslimu na kesi hiyo ikaorodheshwa kusikizwa mnamo Agosti 28, 2019.

Katika mahakama iyo hiyo Charles Ondieki Nyabuto alishtakiwa kwa kumlaghai Bw Maurice Owiti Sh10 milioni akimdanganya alikuwa na uwezo wa kumtolea kontena kutoka bandari ya Mogadishu.

Aliachiliwa kwa dhamana ya Sh1.5 milioni. Kesi itasikizwa mnamo Agosti 12, 2019.