Raia wa India na Mkenya wazuiliwa kwa ulanguzi wa binadamu
Na RICHARD MUNGUTI
WASHUKIWA wawili wa ulanguzi wa binadamu Alhamisi waliamriwa wazuiliwe kwa siku tano.
Raia wa India Bw Patel Ketulkumar Govindbhai na raia wa Kenya Bw Patroba Odhiambo Tobia waliagizwa wazuiliwe katika kituo cha polisi hadi Feburuari 26.
Hakimu mwandamizi Bw Ben Nzakyo aliagiza Bw Govindbhai na Bw Tobia wazuiliwe kuhojiwa na kuwasaidia polisi kuwatambua washukiwa wengine wanaoshirikiana nao katika ulanguzi wa binadamu.
Kiongozi wa mashtaka alikuwa ameomba washukiwa hao wazuiliwe kwa siku 15 katika kituo cha polisi Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA).
Lakini wakili Abdul Agonga anayewatetea washukiwa hao alipinga ombi la washukiwa kuzuiliwa kwa siku 15 akisema idara ya uhamiaji inayowachunguza iko na pasipoti zao na hahiitaji muda huo kuzichunguza.
Bw Agonga aliomba washukiwa hao wawili waachiliwe kwa dhamana akisema, “Kifungu nambari 49 cha katiba kinaruhusu mshukiwa kuachiliwa kwa dhamana uchunguzi ukiendelea.”
Akiwasilisha ombi la kuzuiliwa kwa washukiwa hao kwa siku 15 afisa wa idara ya uhamiaji anayechunguza kesi hiyo Bw Gilbert Awate Walter alisema wawili hao watahojiwa kuhusu ulanguzi wa binadamu kosa ambalo adhabu yake ni faini ya Sh500,000 ama kifungo cha miaka mitatu jela.
Pia alisema idara ya uhamiaji inatazamia kumshtaki kwa kosa lingine la kughushi pasi ya kusafiria na adhabu yake ni faini ya Sh3milioni ama kifungo cha miaka mitano gerezani.
“Ushahidi uliopo sasa ni kwamba washukiwa hawa wanaghushi hati za usafiri za Amerika na kuzibandika katika pasipoti zilizotolewa na Serikali ya Kenya,” alisema Bw Walter.
Mahakama ilifahamishwa washukiwa wametekeleza uhalifu wa kimataifa na mahojiano ya kina yanatakiwa kufanywa.
Akitoa uamuzi Bw Nzakyo alisema “Polisi na maafisa wa idara ya uhamiaji wanahitaji muda kukamilisha uchunguzi kabla ya kuwafungulia mashtaka washukiwa hao wawili.”
Bw Nzakyo aliamuru wawili hao warudishwe kortini Feburuari 26, 2019.