• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 6:50 AM
Raila achomoa kucha na kushambulia serikali baada ya kimya kirefu

Raila achomoa kucha na kushambulia serikali baada ya kimya kirefu

BENSON MATHEKA NA WINNIE ATIENO

KIONGOZI wa Azimio Raila Odinga ameonekana kurejelea ukosoaji wake wa serikali ya Kenya Kwanza licha ya Rais William Ruto kuunga mkono azma yake ya kugombea uenyekiti wa Tume ya Muungano wa Afrika (AUC).

Raila ameanza kurushia lawama uongozi wa Kenya Kwanza akisema umeshindwa kutatua matatizo ya Wakenya hasa mafuriko yanayohangaisha wakazi maeneo mengi nchini.

Tangu alipotangaza azma yake ya uenyekiti wa AUC, Bw Odinga amekuwa akiepuka kukosoa serikali baada ya Rais Ruto kutangaza kwamba Kenya inamuunga mkono waziri mkuu huyo wa zamani kuwania wadhifa wa juu katika barani Afrika.

Hata hivyo, mnamo Ijumaa, Bw Odinga alishambulia vikali serikali ya Kenya Kwanza kwa sera zake ambazo alidai zimeshindwa kutatua shida za raia.

Akionekana kumlenga moja kwa moja Rais Ruto na mawaziri wake, Bw Odinga alisema Kenya Kwanza imekuwa ikiongezea Wakenya mateso kupitia ushuru na kubomoa makazi yao bila mpango.

Akizungumza katika mtaa wa Mukuru Kwa Reuben alipoongoza kikosi cha Azimio kusambazia wahanga wa mafuriko chakula, Bw Odinga alisema iwapo Azimio ingekuwa mamlakani, ingetekeleza mipango ya kuepushia Wakenya mateso msimu huu wa gharika ya mafuriko.

“Sisi kama Azimio tulikuwa na mikakati bora ya kuongoza nchi hii. Zakayo ameshindwa kwa sababu hawakuwa na mpango wowote,” alisema.

Alilaumu serikali kwa kukandamiza haki za raia za kuandamana hasa kwa kuvuruga maandamano ya upinzani mwaka jana.

“Walisingizia eti maandamano yalikuwa yakiwafanya wasitekeleze ajenda yao. Tukasema tukae kando tuone lakini tangu wakati huo hawajafanya chochote. Wamechanganyikiwa, mkono wa kulia haujui wa kushoto unafanya nini. Sisi kama Azimio tulikuwa na suluhisho,” alisema Bw Odinga.

Alilaumu serikali kwa kubomoa nyumba katika mtaa wa Mukuru Kwa Njenga bila kuwapa wakazi makao mbadala na akaahidi kuwaongoza wakazi kupinga mpango huo.

Alilaumu serikali kwa kukosa kutangaza mafuriko kuwa janga la kitaifa ili ipate usaidizi wa kimataifa.

Ilikuwa mara ya kwanza kwa kiongozi huyo wa chama cha ODM kushambulia serikali vikali tangu yeye na Rais Ruto waunde kamati ya kitaifa ya maridhiano na baadaye akatangaza azma ya kugombea uenyekiti wa Tume ya Muungano wa Afrika.

Kauli yake ilikera viongozi wa Kenya Kwanza huku kiongozi wa wengi katika seneti Aaron Cheruiyot ambaye ni mwandani wa Rais Ruto akimlaumu kwa kukosa uungwana hata wakati huu ambapo serikali inamsaidia kupata kazi ya AUC.

Bw Cheruiyot alisema kwamba Bw Odinga haeleweki kuashiria hawakutarajia akosoe serikali kwa kuwa inaunga mkono azma yake. Rais Ruto anaongoza kampeni ya kumpigia debe ili ashinde wadhifa huo katika uchaguzi utakaofanyika mwaka ujao.

Jana, kinara mwenza wa Azimio la Umoja Kalonzo Musyoka aliambia viongozi wa serikali kwamba kumpigia debe Bw Odinga kupata uenyekiti wa AUC hakumaanishi hafai kuzungumzia masuala ya kitaifa.

“Si kwamba kwa kuwa ni suala la kitaifa na anaungwa mkono na serikali anafaa kunyamaza. Bw Odinga hawezi kuzimwa” akasema Bw Musyoka akiwa Mombasa.

Makamu rais huyo wa zamani alisema kwamba Bw Odinga ataendelea kuwa kiongozi wa Azimio hadi atakaposhinda uenyekiti wa AUC.

Bw Musyoka alisema kwamba mafuriko ni suala muhimu kitaifa na ni haki ya Bw Odinga kukosoa serikali kwa kutolishughulikia ipasavyo.

  • Tags

You can share this post!

Mung’aro abadili nia kuhusu ‘kumpelekea...

Uingereza yatoa fedha kusaidia Wakenya wanaohangaishwa na...

T L