Habari MsetoSiasa

Raila ajiandaa kupigia debe kura ya maamuzi

May 14th, 2019 2 min read

Na BENSON AMADALA

KIONGOZI wa ODM, Raila Odinga anajiandaa kuanza msururu wa kampeni kuhimiza wafuasi wake katika eneo la Magharibi, kujiandaa kwa ajili ya mabadiliko ya katiba kupitia kura ya maamuzi.

Hayo yalibainika baada ya Bw Odinga kukutana na Gavana wa Kakamega, Bw Wycliffe Oparanya, Jumapili kijijini Emabole, Butere.

Bw Odinga baadaye alikutana na kundi la madiwani wa Kaunti ya Kakamega ambapo alifichua kuwa ataanza msururu wa mikutano ya kisiasa katika eneo la Magharibi, ili kupigia debe kamati iliyobuniwa kuunda mikakati ya kuunganisha Wakenya (BBI).

Aliwataka madiwani kuunga mkono kamati ya BBI na kujiandaa kwa ajili ya mabadiliko ya katiba kupitia kura ya maamuzi kabla ya uchaguzi mkuu wa 2022.

Eneo hilo sasa huenda likawa uwanja wa mapambano ya kisiasa baina ya Bw Odinga na Naibu wa Rais William Ruto, ambaye amekuwa akizuru Magharibi mara kwa mara kujipigia debe kwa ajili ya uchaguzi wa 2022.

Dkt Ruto amezuru Kaunti ya Kakamega zaidi ya mara kumi tangu Januari mwaka huu, ambapo amekuwa akiongoza mikutano ya kuchangisha fedha.

Dkt Ruto pamoja na wanasiasa wanaomuunga mkono kama vile Seneta wa zamani wa Kakamega, Dkt Boni Khalwale, wamekuwa wakitumia mikutano hiyo ya kuchangisha fedha kujipigia debe.

Dkt Khalwale, ambaye ni naibu kiongozi wa chama cha Ford Kenya, amekuwa akiisihi jamii ya Waluhya kumtelekeza Bw Odinga na badala yake wamuunge mkono Dkt Ruto katika kinyang’anyiro cha urais kwenye uchaguzi mkuu ujao.

Jumapili, Bw Odinga alikutana na Bw Oparanya kwenye kikao cha faragha kwa muda wa zaidi ya saa nne. Baada ya kikao Bw Odinga alionekana mchangamfu lakini hakufichua yaliyojadiliwa.

Kiongozi wa ODM alifululiza hadi kwa kikao na Bw Oparanya mara baada ya kutua kijijini Emabole kwa helikopta.

Kiongozi wa Wengi wa Bunge la Kaunti ya Kakamega, Bw Joel Ongoro, alisema kuwa viongozi hao wawili walitoka kwenye kikao hicho ‘wakionekana wenye furaha na wachangamfu’.

“Bw Odinga alituhutubia kwa ufupi na kutuhimiza kuunga mkono mipango ya kutaka kubadili katiba kupitia kura ya maamuzi,” akasema Bw Ongoro.

Mwakilishi wa Kike Kaunti ya Kakamega, Bi Elsie Muhanda, alisema Bw Odinga na Bw Oparanya walikutana kwa zaidi ya saa nne na kabla ya kuhutubia viongozi wa kaunti waliofika kumlaki.

“Inaonekana Bw Odinga na Gavana Oparanya wameanza mikakati ya kuandaa vikosi vyao kabla ya kuanza kampeni ya kupigia debe mabadiliko ya katiba kupitia kura ya maoni,” akasema Bi Muhanda.