Habari Mseto

Raila amtembelea Joho kumjulia hali

November 17th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na WANDERI KAMAU

KINARA wa Chama cha ODM, Bw Raila Odinga, Jumamosi alimtembelea Gavana wa Mombasa, Bw Hassan Joho nyumbani kwake katika mtaa wa Vipingo akisema alienda kumjulia hali gavana huyo baada ya kuugua kwa muda.

Bw Joho alilazwa hospitalini Mombasa wiki iliyopita baada ya kuugua malaria.

“Leo (Jumamosi) nimemtembelea Bw Joho nyumbani kwake kumtakia afua ya haraka na nimefurahishwa na hali yake ya afya,” akasema Bw Odinga kwenye taarifa fupi.

Wiki iliyopita, gavana huyo pia alitembelewa na aliyekuwa rais wa Nigeria, Bw Olusegun Obasanjo.

Ziara ya Bw Odinga inajiri wakati hatua za Bw Joho katika uongozi wa kaunti hiyo zinatazamwa kwa makini.

Mapema wiki iliyopita, mawaziri wote 10 wa kaunti walipoteza kazi ikisemekana kandarasi zao zimeisha.

Serikali ya Bw Joho haijatangaza nafasi hizo kuwa wazi, kama inavyotakikana kisheria.

Majukumu ya mawaziri hao sasa yanatekelezwa na makatibu katika wizara zao.

Madiwani

Gavana huyo pia hajawa na uhusiano mzuri na madiwani katika Bunge la Kaunti hiyo, ambao wengi ni wanachama wa ODM.

Hivi majuzi, madiwani waliibua mjadala wakisema gavana huyo amewasahau kwani hajaenda kutoa hotuba yake katika bunge la kaunti mwaka huu.

Magavana huhitajika kutoa hotuba mara moja kila mwaka bungeni kuhusu hali ya kaunti.

Vilevile, ziara ya Bw Odinga imetokea wakati ambapo baadhi ya wakazi wanazidi kumkashifu gavana huyo kwa kimya chake kuhusu mzozo wa usafirishaji mizigo kwa reli ya SGR kutoka bandarini.