Raila, Mudavadi wamwomboleza Nginyo Kariuki
Na CHARLES WASONGA
KIONGOZI wa ODM Raila Odinga amemwomboleza mwanasiasa na mfanyabiashara mashuhuri Nginyo Kariuki kwa kumtaja kama mzalendo na kiongozi ambaye alichangia pakubwa katika harakati za kupigania utawala wa kidemokrasia nchini.
Kariuki alifariki Jumatano asubuhi katika Hospitali ya Agha Khan, Nairobi ambako alikuwa amelazwa akipokea matibabu.
“Rambi rambi zangu ziendee familia, jamaa na marafiki wa mfanyabiashara na mwanasiasa Nginyo Kariuki ambaye alifariki leo (Jumatatu) asubuhi. Mzee Nginyo alitoa mchango mkubwa zaidi katika mapambano ya kidemokrasia nchini. Mungu aifariji familia yake katika kipindi hiki kigumu,” Bw Odinga akasema kupitia akaunti yake yake ya Twitter.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka familia, mwanasiasa huyo alifariki mwendo wa saa nane za usiku wa kuamkia Jumatatu.
Kiongozi wa ANC Musalia Mudavadi pia ameombeleza familia ya marehemu.
Amemtaja Kariuki katika mfanyabiashara shupavu na ambaye alihusudu mchezo wa gofu.
“Nimehuzunisha na kifo cha Nginyo Kariuki mfanyabiashara na mawanasiasa shupavu ambaye alipigania kurejelewa kwa utawala wa vyama vingi nchini. Na katika Nyanja ya michezo alikuwa mchezaji hodari wa gofu. Natuma rambirambi zangu kwa familia yake na Mungu aiweke roho yake pema penye utulivu,” Bw Mudavadi akasema kipitia Twitter.
Marehemu Kariuki alikuwa mwanachama mwanzilisha wa chama cha The National Alliance (TNA) mnamo 2012; na ambacho kiliunga na chama United Republican Party (URP) kubuni muungano wa Jubilee ulioshinda katika uchaguzi mkuu wa 2013.
Hadi kifo chake amekuwa msemaji wa chama cha Jubilee katika Kaunti ya Kiambu.
Mnamo Agosti mwaka jana, Mzee Kariuki aliwasilisha maoni na mapendekezo yake kwa jopo la maridhiano (BBI).