• Nairobi
  • Last Updated May 10th, 2024 2:21 PM
Rais afichua gumzo lake la mwisho na Collymore

Rais afichua gumzo lake la mwisho na Collymore

Na LEONARD ONYANGO

ALIYEKUWA Afisa Mkuu Mtendaji wa Safaricom, marehemu Bob Collymore alimwambia Rais Uhuru Kenyatta wiki chache kabla ya kuaga dunia kuwa alikuwa amefika mwisho wa maisha yake.

Akizungumza wakati wa misa ya wafu katika kanisa la All Saints Cathedral jijini Nairobi jana, Rais Kenyatta alisema Bw Collymore alimuomba atunze mkewe Wambui Kamiru Collymore na watoto wake.

“Nahisi nina wiki chache tu za kuishi. Nimefika mwisho. Nimejaribu kila kitu na sasa nimekubali kuwa wakati wangu umefika. Huwezi kufanya chochote kunisaidia. Nimepanga maisha yangu. Kile tu unaweza kufanya ni kulinda Wambui na watoto wangu,” akasema Rais Kenyatta kuhusu mazungumzo yake na Bw Collymore kabla ya kuaga dunia.

Bw Collymore alifariki mnamo Jumatatu kutokana na kansa ya damu, na mwili wake ukachomwa siku iliyofuata jijini Nairobi.

Aliacha mjane Wambui na watoto wanne.

Rais Kenyatta alikuwa ziarani nchini Canada wakati mwendazake Collymore alimpigia simu akitaka kumweleza kwamba siku zake duniani zilikuwa zinaendelea kuisha.

“Alinipigia simu kwa mara ya kwanza usiku wa manane nikiwa Canada. Sikushika simu kwa sababu ilikuwa saa nane usiku. Siku ya pili alinipigia tena nikaamua kuzungumza naye,” akasema Rais Kenyatta.

Wajadili

Hatimaye Rais aliporejea kutoka Canada alikutana na Collymore katika Ikulu ili wajadili kwa kina kilichokuwa kikimsumbua mkuu huyo wa Safaricom.

“Kuna vitu vinne ambavyo Collymore alipenda. Kitu cha nne siwezi kusema hapa. Bob alipenda Kenya, kampuni ya Safaricom na Bob alipenda mke na watoto wake. Nilisema kitu cha nne siwezi kusema hapa,” akasema Rais Kenyatta.

“Nilizungumza na Bob kwa muda wa saa tatu ambapo alinieleza maono yake katika kampuni ya Safaricom na Kenya kwa ujumla.”

Aliendelea: “Kadhalika, Bob alinieleza ninavyoweza kukabiliana na ufisadi na akanihimiza kutolegeza kamba. Kwa heshima ya Bob nitahakikisha kuwa ufisadi umeangamizwa,” akasema Rais Kenyatta.

Naibu Rais William Ruto alimtaja Collymore kama mchapakazi aliyechangia katika maendeleo.

  • Tags

You can share this post!

Mnada: Wengi wafika kituo cha polisi Thika kununua magari...

Macho ya Wakenya kwa Timothy Cheruiyot mbio za Diamond...

adminleo