• Nairobi
  • Last Updated May 21st, 2024 5:29 PM
Rais aongoza Wakenya kuomboleza afisa wa NCIC

Rais aongoza Wakenya kuomboleza afisa wa NCIC

Na FADHILI FREDRICK na WACHIRA MWANGI

RAIS Uhuru Kenyatta aliongoza Wakenya kuomboleza kifo cha Naibu Mwenyekiti wa Tume ya Uwiano na Utangamano (NCIC) Fatuma Tabwara aliyeaga dunia Jumapili katika Kaunti ya Kwale.

Bi Tabwara aliaga dunia kabla ya mwezi mmoja tangu aapishwe.

Katika risala yake, Rais Kenyatta alimtaja Tabwara kama shujaa aliyepigania haki za wanawake na wasichana hasa kaunti ya Kwale.

“Inasikitisha sana kwamba tumempoteza mmoja wa viongozi waliokuwa na nia ya kuleta mazuri katika eneo la Pwani. Wakati huu wa majonzi na huzuni, nawasilisha pole zangu na risala za rambirambi za dhati kwa jamaa, ndugu na marafiki,” kasema Rais Kenyatta,” akasema Rais Kenyatta.

Naibu mwenyekiti huyo wa NCIC alizimia na kufariki wakati wa sherehe ya arusi ya jamaa yake aliyokuwa amehudhuria kijijini Bowa wilayani Matuga katika Kaunti ya Kwale.

Kulingana na mwanawe Said Fuad, Bi Tabwara alikuwa na matatizo ya shinikizo la damu. Bw Fuad alisema mamake aliwahiwa hospitali ya Diani Beach ambapo aliaga dunia.

Alisema alipokea taarifa kuhusu kifo cha mama yake saa 4.00 asubuhi Jumapili.

“Amekuwa na tatizo la shinikizo la damu kwa muda mrefu lakini alionekana mwenye afya alipoenda harusini. Lakini kwa bahati mbaya alizimia na kufariki dunia alipokuwa akitibiwa hopsitalini,” akasema.

Gavana wa Kwale Salim Mvurya alisema kuwa alikuwa na mwendazake katika harusi nyingine Jumamosi na alikuwa buheri wa afya na mchangamfu.

“Jumamosi alikuwa miongoni mwa wageni wa heshima katika harusi nyingine. Alionekana mwenye nguvu na mchangamfu. Nilizungumza naye kwa takribani dakika 10,” akasema Gavana Mvurya.

You can share this post!

Uhuru atabaki katika uongozi baada ya 2022, adai Murathe

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Uigaji hauzuiliki katika ubunifu...

adminleo