Rais ataja marehemu Moi kama shujaa
Na BENSON MATHEKA
RAIS Uhuru Kenyatta, jana aliongoza viongozi wa Afrika kummiminia sifa aliyekuwa rais wa pili wa Kenya hayati Daniel arap Moi kwa mchango wake wa kuhubiri amani, upendo na upatanishi.?
Marais wa mataifa saba na viongozi 18 wa serikali za kigeni walihudhuria ibada ya kumkumbuka Mzee Moi katika uwanja wa michezo wa Nyayo jijini Nairobi.
“Leo nimeamua kutoomboleza kufariki kwa shujaa bali kusherehekea kiongozi na simba wa historia,” akasema Rais Kenyatta.
Waliozungumza katika ibada hiyo walisema kwamba waliungana na Wakenya kusherehekea maisha ya kiongozi shujaa na mzalendo aliyependa Afrika.
Rais Kenyatta alisimulia kuhusu mchango wa Moi kwa nchi hii akiwa mpiganiaji uhuru, mbunge, waziri, makamu wa rais na rais na kusema hawezi kusahaulika kamwe.
“Kutoka maisha yake ya ujana, Moi alielewa thamani ya Kenya kuwa kubwa kuliko mtu binafsi. Alipotakiwa kuhudumia nchi, Mzee Moi alihudumu akiwa mnyenyekevu na kwa bidii kusaidia kuunda Kenya ya sasa yenye ustawi,” akasimulia Rais Kenyatta.
Alimsifu Moi akisema aliweka msingi kwa kukubali kuondoka mamlakani alipokabidhi mamlaka kwa amani 2002.
Alimtaja Moi kama kiongozi aliyekuwa na maono yaliyomwezesha kutawala kwa miaka 24 akitenda aliloweza kulinda Kenya.Alisema Moi alionyesha mfano mwema wa uongozi kwa kukubali kuondoka mamlakani 2002.
“Wakenya walipofanya uamuzi wao 2002, aliamua kukubali mapenzi yao na akaongoza chama chake kuwa upinzani. Alikuwa akitukumbusha kuwa upinzani sio adui wa nchi bali ni serikali inayosubiri kuingia mamlakani; na tunafaa kuwa waaminifu kwa nchi, kwa kuweka mikakati ya kuimarisha amani, upendo na umoja wa Wakenya,” Rais Kenyatta alisema.
Alisema Moi atakumbukwa kwa kuongoza nchi kupiga hatua katika elimu, kuwapa uwezo wanawake na kubadilisha utumishi wa umma.
“Tunamshereheka Mzee Moi kwa kubadilisha sekta ya elimu kupitia mfumo wa 8-4-4 ambao tumeupatia nguvu zaidi kupita mtaala mpua wa Competence Based Curriculum,” alisema.
Aliwahimiza Wakenya kuiga Mzee Moi ambaye amesifiwa na wengi kwa kuwa mchapa kazi. “Maono ya Rais Moi kuhusu Kenya hutuhimiza tuendelee kufanya kazi bila kuchoka ili kuwa na uwezo wa kutuinua kama taifa kufikia viwango vya juu vya umoja, ustawi na demokrasia,” alishauri Rais.
Katika hotuba yake iliyokuwa kilele cha ibada ya kitaifa ya kumkumbuka hayati Moi, Rais Kenyatta alisema rais huyo wa pili wa Kenya alisaidia nchi nyingi kupata amani.
Alitaja nchi alizoongoza juhudi za upatanishi kama Uganda, the Sudan, Sudan Kusini, Ethiopia, Eritrea, Somalia, Rwanda, Jamhuri ya Demokrasia ya Congo na Burundi. Rais alisema chini ya utawala wa Moi, Kenya ilikomaa kisiasa na kukumbatia demokrasia ya vyama vingi.
“Ilikuwa wakati wa utawala wake ambapo Kenya ilirejelea siasa za vyama vingi, mfumo ambao mwaka wa 1991, Moi alionya kuwa unaweza kugawanya Wakenya usiposimamiwa vyema na kuainishwa na utamaduni, historia na malengo yetu,” alisema.
Haikuwa rahisi kwa Moi kubali mfumo wa vyama vingi vya kisiasa na alikubali baada ya shinikizo kutoka kwa upinzani, wanaharakati na jamii ya kimataifa.
“Kenya ni bora kwa kuwa na Mzee Daniel Toroitich arap Moi kama mwana wake, mtumishi, kiongozi wake na mfano wa kuigwa. Sote tunapaswa kujifunza kutoka safari ya maisha yake,” alisema.
Alisema ingawa Moi atazikwa leo, ataendelea kuishi miongoni mwa Wakenya: “Hakika, tumekuja, sio kuomboleza kifo chake lakini kusherehekea maisha ya shujaa wa historia.”