Rais atoa sifa kedekede kwa mwendazake Matiba
Na BENSON MATHEKA
RAIS Uhuru Kenyatta Jumatano aliongoza Wakenya kumuaga aliyekuwa mpiganiaji shupavu wa demokrasia ya vyama vingi nchini Kenneth Matiba katika ibada ya wafu iliyohudhuriwa na viongozi wa NASA.
Rais Kenyatta alimtaja marehemu Matiba kama mwanasiasa shupavu ambaye Wakenya hawataweza kumsahau.
“Ken Matiba ni nembo ya jinsi Kenya inapaswa kuwa. Alikuwa amejiotolea kufanya kazi kwa bidii na alikuwa tayari kutoa mali na utajiri wake wote kafara kwa ajili ya nchi hii,” alisema Rais Kenyatta.
Kuonyesha jinsi alivyomheshimu marehemu Matiba, Rais Kenyatta aliungana na familia na marafiki kubeba jeneza lililokuwa na mwili wake kutoka ndani ya kanisa la All Saints Cathedral hadi gari la kubeba maiti nje ya kanisa hilo.
Alisema itakuwa vigumu kwa Wakenya kumsahau Matiba kwa ujasiri wake alipopigania demokrasia ya vyama vingi miaka ya tisini. Rais alisema kuna somo la Wakenya kujifunza katika maisha ya Matiba na hasa viongozi wanaofaa kujiuliza watakachokumbukwa nacho.
“Kenya itamkosa lakini haitamsahau kamwe,” alisema na kuwataka viongozi kuwalea vijana ambao watawarithi alivyofanya Bw Matiba kisiasa.
“Viongozi wa kweli hawaogopi kuwalea na kuwafunza wengine watakaowarithi,” alisema Rais Kenyatta.
Akihutubia waombolezaji, Naibu Rais William Ruto alimtaja Matiba kama shujaa ambaye kujitolea kwake kupigania demokrasia ili kufaidi wengi.
“Baadhi yetu tulikuwa wachanga na hatukuweza kupata nafasi ya kumjua Matiba binafsi lakini tumenufaika na kujitolea kwake kupigania demokrasia,” alisema Bw Ruto.
Aliongeza: “Ni kwa sababu ya kujitolea kwa Matiba na wengine ambako kulifanya Kenya kuwa demokrasia yenye uhuru zaidi ambayo watu kutoka kote wanaweza kuchangia katika uongozi wa nchi.”
Familia ya Matiba na marafiki walimtaja kama aliyekuwa kiongozi na mfanyabiashara mkarimu katika maisha yake. Mjane wake Edith alisema ukarimu wa Matiba haukuwa na mipaka.
“Ken alitaka hadhi, uhuru wa kifedha na haki kwa kila Mkenya,” alisema. Rafiki wa miaka mingi wa Matiba Bw Joseph Kibe alisema marehemu alikuwa akiongoza kwa kutekeleza aliyoamini na aliyotaka watu wengine wafanye.
“Matiba hakuamini katika kurudi nyuma kamwe. Kila wakati alikuwa katika msitari wa mbele na hakuvumilia kazi duni,” alisema.
Bw Marsden Madoka ambaye alihudumu katika serikali pamoja na Matiba alikumbuka mapenzi ya marehemu kwa spoti. “Aliamini kuwa spoti inaweza kuunganisha Wakenya,” alisema.
Rais mstaafu Mwai Kibaki, vinara wa NASA Musalia Mudavadi, Kalonzo Musyoka, Moses Wetangula na kiongozi wa chama cha Narc Kenya Martha Karua pia walihudhuria ibada hiyo.
Ibada kama hiyo itafanyika katika Muranga leo kabla ya mwili wake kusafirishwa hadi Nairobi kuteketezwa ili kutimiza matakwa yake.