Rais aweka kando itifaki na kumruhusu Sonko kuhutubu
Na MARY WANGARI
RAIS Uhuru Kenyatta kwa mara nyingine aliibua gumzo miongoni mwa Wakenya kufuatia hatua yake ya kukatiza ghafla hotuba yake na kumruhusu Gavana Mike Sonko kuwahutubia wananchi Jumamosi, Julai 20, 2019.
Rais alikuwa amehudhuria maadhimisho ya Siku ya Ushirika yaliyoandaliwa Kenyatta International Convention Centre (KICC) Nairobi.
Ni hapo ndipo aliamua kukiuka kanuni za utaratibu rasmi na kumruhusu Gavana wa Nairobi kuwahutubia wananchi.
“Lakini kabla ya ninene kidogo, wajua kila mji una mwenyewe, sitaki afikirie kwamba nimemsahau. Acha nimruhusu hapa gavana Sonko azungumze kisha tuendelee,” alisema Rais Kenyatta huku wananchi wakimshangilia kwa kitendo hicho kilichoonyesha unyenyekevu.
Sonko ambaye bila shaka alifurahishwa na fursa hiyo ya kipekee ambayo hakuitarajia alimshukuru rais kwa heshima hiyo.
“Sitaki kusema mengi kwa sababu Rais akisimama hakuna mtu mwingine yeyote anapaswa kuzungumza. Hiyo ni heshima kubwa sana ambayo Rais ametupatia,” alisema Gavana huyo wa Nairobi.
Itifaki
Hatua hiyo ya Rais Uhuru iliwashangaza wengi kwa kuwa ni kinyume na utaratibu rasmi kuhusu mpangilio wa hotuba katika mikutano inayohudhuriwa na rais na wajumbe wa serikali.
Kwa kawaida, hotuba katika mikutano kama hiyo huwa zinafuata utaratibu maalumu.
Kulingana na kanuni za utaratibu huu, hotuba hutolewa katika mpangilio wa kutoka chini hadi juu ambapo Rais ndiye anayepaswa kuwa wa mwisho kuzungumza na hakuna mtu mwingine anayeruhusiwa kuzungumza baada yake.
Hivyo basi, katika hafla hii, ilitarajiwa kwamba hotuba ya Uhuru ndiyo ingekuwa ya mwisho.
Hata hivyo, hii si mara ya kwanza kwa Rais Uhuru ambaye ni mwepesi wa kuingiliana na raia na hata kufanya kinyume na matarajio ya utaratibu rasmi huku baadhi ya visa vikiwaacha wengi vinywa wazi.
Mnamo Januari 20, Uhuru alikiuka kanuni za utaratibu alipoacha ndege iliyokuwa ikimsubiri pamoja na walinzi wake na kutoweka kwa gari pamoja na kiongozi wa Orange Democratic Movement, ODM mahali pasipojulikana mjini Kisumu.
Rais pia alikiuka kanuni alipomkumbatia kiongozi wa upinzani, Raila mnamo Aprili 17.
Mnamo Septemba 2016, Kiongozi wa Taifa aliibua hisia kali baada ya kumruhusu msanii wa nyimbo za injili kuketi kwenye kiti chake wakati wa hafla.