Rais Kenyatta kuamua hatima ya mtoto aliyemuua yaya
Na RICHARD MUNGUTI
KATIKA kesi ya aina yake mvulana mwenye umri wa miaka 19 aliyepatikana na hatia ya kuua alipokuwa na umri wa miaka 15 aliamriwa Jumatano azuiliwe katika gereza kuu la Kamiti hatima yake itolewe na Rais Uhuru Kenyatta.
Jaji Jessie Leesit aliyempata na hatia Erick Kimeu Kimani alisema sheria ya kutetea haki za watoto haimruhusu kupitisha adhabu ya kifo dhidi yake (kimani) bali inamkubalia aagize azuiliwe gerezani “kwa hiari ya Rais.”
Faili ya mshtakiwa itakuwa inapelekwa kwa mbele ya Rais kila baada ya miaka mitatu atoe mwelekeo.
Jaji Leesit alisema Kimani alitekeleza uhalifu huo akiwa na umri wa miaka 15 na kushtakiwa kwa kosa hilo ambayo hukumu yake ni kifo au kifungo cha maisha gerezani.
Kimani alishtakiwa kumuua mjakazi wao mwenye umri wa miaka minane unusu Bi Rose Ann Wanje na kutupa mwili wake kwenye shamba la mahindi katika kijiji cha Kawaida katika kaunti ya Kiambu mnamo Agosti 21 2014.
Jaji Leesit alielezwa na mashahidi 11 walioitwa na kiongozi wa mashtaka Bi Evelyn Onunga kuwa Wanje aliyekuwa ameajiriwa kumtunza mtoto wao (kimani) aliyekuwa na umri wa miaka minne.
Ijapokuwa mshtakiwa alikuwa amekanusha mashtaka dhidi yake Jaji Leesit alisema ni yeye (kimani) aliyekuwa mtu wa mwisho kuonekana akiwa na marehemu akiwa hai siku hiyo aliyoripotiwa ametoweka.
“Ni wewe ulimuua Wanje na wala sio watu wengine kama unavyodai. Hausingiziwi ulimuua Wanje kama unavyodai bali ni wewe uliyehusika na mauaji hayo. Sina tasishwi akilini mwangu kuwa ni wewe ulitekeleza uhalifu huo,” alisema Jaji Leesit akitoa uamuzi jana.
Mahakama ilisema mshtakiwa na Yaya huyo walionekana wakiandamana kumtafuta ndugu yao mdogo kwa jirani yao wamrudishe kwa nyumba wampe chakula.
Jaji Leesit alisema ushahidi uliowasilishwa na Bi Onunga aliyeshirikiana na wakili wa Seriakli Bi Grace Njuguna ulimlenga Kimani tu.
Mahakama ilisema ijapokuwa mshtakiwa amejaribu kujinasua kamba za ushahidi zimemfunga kabisa kwenye kesi hii
Jaji Leesit alisema mshtakiwa aliandika barua ya vitisho na kuibandika kwenye mlango wa jirani yao akitisha kuwaangamiza jinsi “alimwangamiza Bi Wanje.”
Barua hiyo ilipewa maafisa wa Polisi ndipo mshtakiwa akatiwa nguvuni na kufunguliwa mashtaka ya kumuua Bi Wanje.
“Nimeridhishwa na ushahidi uliowasilishwa katika kesi hii na upande wa mashtaka umemlimbikizia lawama mshtakiwa.Hakuna mtu mwingine ambaye alihusika na mauaji ya Wanje ila wewe,” Jaji Leesit alisema akitoa uamuzi.
Mahakama ilisema kuwa mshtakiwa aliandika barua yenye vitisho akisimulia jinsi mwendazake alivyouawa.
“Mshtakiwa alificha kabisa kisa hiki hadi alipotiwa nguvuni na kuhojiwa na mawakili wa Serikali ndipo ilibainika alichokitenda,” alisema Jaji Leesit.