Habari Mseto

Rais 'matatani' kuhusu kura ya maamuzi

June 4th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na MWANGI MUIRURI

RAIS Uhuru Kenyatta yuko katika njia panda kuhusu kura ya maamuzi ya mabadiliko ya katiba huku mirengo miwili mikuu ya kisiasa nchini ikimweka pembeni kwa masharti.

Huku Rais akishikilia handisheki yake na Raila Odinga kuleta uthabiti wa utawala wake katika awamu hii ya pili na ya mwisho, na akijaribu kutunza uthabiti ndani ya serikali yake katika mkataba wa maelewano na mrengo wa Naibu Rais Dkt William Ruto, siasa za referenda zinaonekana kumzubaisha na kumuacha ‘kwenye mataa’ kisiasa.

Shida kuu ni kwamba, mirengo hii miwili inalumbana vikali ikihujumiana waziwazi, Rais naye akionekana kutokuwa na mstakabali wa kuendeleza chama chake cha Jubilee katika siasa za urithi wa 2022 hivyo basi kuzua hali ya kuchanganyikiwa katika ngome za Jubilee.

Tena, Rais akionekana kulenga kuondoka afisini ifikapo mwaka 2022 akiwa na nembo ya kuunganisha Wakenya, suala hili la referenda halijapata uwiano wa hasa nini kinafaa kibadilishwa.

Wakati mrengo wa Odinga unapendekeza kupanuliwa kwa vyeo vya kugawanwa, Ruto anapinga kuundwa kwa vyeo nayo makundi ya kijamii yana mapendekezo chungu nzima; hivyo basi kuweka Rais katika njia panda ya uhakika.

Hali ni mbaya kwake kiasi kwamba tayari dokezi katika serikali kwa Taifa Leo zimefichua kuwa idara ya ujasusi nchini (NIS) imempa tahadhari kuwa siasa za sasa ambazo zinaendelezwa huku jina lake liking’ang’aniwa kutumiwa kama idhini ya urithi wa 2022 ni hatari kwa msingi wa amani.

Tayari, wandani wa Raila Odinga ambao hujumuika katika ‘Team Handshake’ wakiongozwa na mbunge wa Ruaraka, Tom Kajwang’ wamesema kuwa “mpende msipende tunaelekea kwa kura ya maamuzi na tuko na idadi tosha ya wapigakura kupitisha maazimio yetu.”

Akiongea Jumapili, Kajwang’ alisema: “Wafuasi wa Ruto na mrengo wake waelewe kuwa Rais Kenyatta na kiongozi wetu Raila ndio wako na ufuasi wa kisiasa hapa nchini. Wakiunganisha wafuasi wao pamoja, tutapitisha malengo yetu ya mabadiliko ya katiba.”

Hata hivyo, Spika wa Bunge la Kitaifa, Justin Muturi alisema kuwa “kuna wanasiasa wanaeneza ndoto kuwa ni rahisi kwa sasa kuandaa kura hiyo.”

Akasema: “Nataka kuwapa onyo kuwa hata Rais Kenyatta anajua kuwa kwa sasa hatuna sheria za kuongoza kura hiyo na haijulikani kama sheria hizo zinaweza kuwa maarufu katika ukumbi wa mabunge yote nchini kuandaa sheria hizo.”

Bw Muturi alisema kwa sasa migawanyiko iliyoko katika siasa za Kenya inatia wasiwasi kuhusu maandalizi ya kura hiyo kwa kuwa ni lazima kwanza kukumbatiwa kwa umoja na nusu ya mabunge yote ya Kaunti na pia seneti na bunge la kitaifa.

Mabunge hayo kwa sasa yamegawanyika katika mirengo ya Kieleweke, Handisheki, na ule wa Ruto na walio na imani kwa vyama vingine vya kisiasa hivyo basi kuzua mng’ang’ano mkuu.

Kuunda vyeo

Tayari, Dkt Ruto amesema kuwa hataunga mkono wito wa kubadilisha katiba ikiwa nia kuu itakuwa ni kuunda vyeo vya kugawana mamlaka ya serikali.

Amesema kuwa Kenya ya sasa ni lazima ikombolewe kutoka kwa siasa za wachache kusaka makuu ya kugawana keki ya kitaifa hadi ziwe kuhusu manufaa ya Wakenya wote kwa ujumla.

“Wengi husema kuwa siko tayari kuungana na Wakenya katika kutekeleza kura ya maamuzi ili tubadilishe katiba eti tupanue nyadhifa za ugavi mamlaka. Huo si uongo. Siwezi nikaunga mkono kura ya maamuzi ambayo itaandaliwa kwa msingi huo,” akasema.

Dkt Ruto akionekana kumlenga Bw Odinga, alisema kuwa “hizi siasa za eti ni lazima mtu fulani afurahishwe ndio kuwe na amani, ni lazima mtu huyu akianguka kura ahifadhiwe katika wadhifa au yule ndio atuhakikishie amani ni lazima agaiwe kipande cha serikali ni kiini cha ghasia za baada ya uchaguzi.”

Dkt Ruto alisema kuwa ataunga kura ya maamuzi ambayo nia yake ni kuleta usawa wa ugavi wa raslimali, uthabiti wa masuala kama vile mishahara na pia usawa wa kijinsia katika ugavi wa mamlaka.