Habari Mseto

Rashid Echesa akosa kufika mahakamani kwa mara ya pili

March 21st, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA RICHARD MUNGUTI

ALIYEKUWA waziri wa Michezo Rashid Echesa aliyeamriwa na Mahakama kuu ashtakiwe upya mnamo Machi 4,2024 hakufika kortini kwa mara ya pili kujibu kesi katika kashfa ya silaha za Sh39.5 bilioni.

Wakili Duncan Okatchi anayemwakilisha Bw Echesa alieleza mahakama ya Milimani kwamba waziri huyo wa zamani alikuwa hajihisi vyema na alikuwa ameshauriwa na daktari apumzike.

“Mshtakiwa hakuweza kufika kortini kwa vile si buheri wa afya. Naomba kesi inayomkabili itajwe baada ya mwezi mmoja apate nafuu,” Bw Okatchi aliisihi mahakama.

Wakati kesi hiyo ilipotajwa mbele ya hakimu mwandamizi Robinson Ondieki, Bw Echesa aliye pia mwenyekiti wa Bodi ya Kenya Water Towers Agency, hakufika ila washukiwa wenzake walikuwa kortini.

Jaji Kanyi Kimondo aliyesikiliza rufaa iliyowasilishwa na Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) akipinga kuachiliwa kwa Bw Echesa na wenzake Februari 2020 alisema hakimu mwandamizi Bw Kennedy Cheruiyot aliyesikiliza kesi iliyomkabili waziri huyo wa zamani, alikosea kutochambua ushahidi wa baadhi ya mashahidi.

“Baada ya kutathmini ushahidi uliowasilishwa na DPP katika kesi iliyomkabili Bw Echesa na wenzake, nimeng’amua kuna ushahidi ambao haukuchambuliwa ipasavyo wa baadhi ya mashahidi,” alisema Jaji Kimondo.

Kufuatia uamuzi huo, Jaji Kimondo aliwaamuru Mabw Echesa, Daniel Otieno, Clifford Okoth, Kennedy Oyoo na Chrispin Oduor wajisalamishe mbele ya Bw Ondieki kupokea maagizo zaidi kuhusu kesi hiyo.

Kutofika kwa Bw Echesa kulisababisha kesi hiyo kuagizwa itajwe tena mnamo Machi 20, 2024.

Jaji Kimondo aliamuru washukiwa hao walioachiliwa na Bw Cheruiyot kufunguliwa mashtaka mapya ya kughushi stakabadhi.

Waliposhtakiwa hapo awali Echesa, Otieno,Okoth,Oyoo na Oduor walikabiliwa na mashtaka ya kula njama kumlaghai raia wa Amerika wakidai wangemsaidia kushinda zabuni ya kuuzia idara ya ulinzi silaha kwa gharama ya Sh39.5 bilioni.

Pia walikabiliwa na shtaka la kupokea pesa kwa njia ya udanganyifu na kupeana hati feki.

Rais Ruto alimteua Bw Echesa kuwa mwenyekiti wa bodi ya Kenya Water Towers Agency mnamo Mei 2023.

Bw Echesa na wenzake walikuwa wameshtakiwa kuwalaghai wawekezaji kutoka Amerika na Misri katika kashfa hiyo ya silaha.

Washtakiwa hao walikabiliwa na mashtaka 12 ya ughushi wa stakabadhi, kupokea pesa kwa njia ya undanganyifu na kujifanya kuwa maafisa wakuu walioajiriwa katika Idara ya Jeshi (KDF).

Walishtakiwa kwamba kati ya Oktoba 2 2019 na Feburuari 13,2020 walijaribu kumlaghai Stanley Bruno Sh39.5bilioni wakidai atapewa zabuni ya kuuzia idara ya ulinzi –DoD silaha.

Ushahidi uliowasilishwa mbele ya Bw Cheruiyot ulisema mikutano kuhusu zabuni hiyo ilifanyika katika jumba lililokuwa na afisi za Rais William Ruto alipokuwa Naibu Rais katika Serikali ya Jubilee.