Habari Mseto

Red Cross yatetewa na wabunge

April 14th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na KALUME KAZUNGU

WABUNGE wanne wa kitaifa wamejitokeza kuwakashifu baadhi ya wanasiasa na Wakenya wanaopiga vita Shirika la Msalaba Mwekundu (Red Cross) kwa madai kwamba shirika hilo limekuwa likiendeleza ubadhirifu wa fedha za kuwasaidia wanaokabiliwa na majanga nchini.

Wabunge Abdulswamad Shariff Nassir (Mvita), Ahmed Abdisalan (Wajir Kaskazini), Mohamed Dahir (Dadaab) na Mwakilishi Mwanamke wa Lamu, Bi Ruweida Obbo, walitaja matamshi ya baadhi ya wanasiasa nchini kuhusu shirika hilo kuwa yasiyofaa.

Wakizungumza eneo la Lamu, wabunge hao walisema kamwe hawajaridhishwa na kupigwa vita kwa shirika hilo walilolitaja kuwa na wanachama waliojitolea kikamilifu kusaidia Wakenya kila mara wanapokumbwa na majanga nchini.

Baadhi ya wanasiasa wamekuwa wakishinikiza kujiuzulu kwa Katibu Mkuu wa Shirika hilo, Bw Abbas Gullet, kwa kile walichokitaja kuwa kufeli kwa shirika hilo katika kukadiria matumizi ya fedha zilizochangwa mnamo 2011 kupitia mpango wa Kenyans for Kenya Fund Drive Initiative.

Shinikizo za wanasiasa hao na Wakenya, hasa watumiaji wa mitandao ya kijamii za kutaka Bw Gullet kujiuzulu zilianza baada ya shirika hilo kuomba fedha zaidi kuchangwa ili kuwasaidia wananchi wanaokabiliwa na baa la njaa katika kaunti zilizoathiriwa na janga hilo.

Katika mazungumzo wakati wa ziara yao Lamu, wabunge walishikilia kuwa wanasiasa wanaoingilia utendakazi wa shirika hilo ni wabinafsi na kwamba wanafanya hivyo ili kuficha maovu yao.

Bw Abdulswamad alisema katu hawatasita kulitetea shirika hilo, akisisitiza kuwa majukumu yake yanajidhihirisha wazi kila unapotembea nchini.

“Wale wanaovamia shirika la Msalaba Mwekundu na kashfa zisizo na maana wakome. Sisi wenyewe kama Wakenya tumejionea mambo mengi mazuri yanayotekelezwa na shirika hilo.

“Najua kuna sakata mbalimbali ambazo zinachunguzwa nchini, ikiwemo wizi wa fedha za ujenzi wa mabwawa na mambo mengine ambayo ni ya kweli. Ikiwa wanasiasa wanajaribu kukimbilia kupiga vita shirika la msalaba mwekundu wakidhani ni rahisi kwao kufanya hivyo, wajue wamepotoka.

“Waache shirika kufanya kazi yake na wasiingize siasa. Tutasimama na kulitetea shirika hilo bila kujali lolote kwani limedhihirisha uwazi na uwajibikaji wa hali ya juu katika utendakazi wake kote nchini,” akasema Bw Abdulswamad.

Bw Abdisalan aliwataja wale wanaoliandama shirika la Msalaba Mwekundu kuwa watu wasio na utu. Alisema maafisa wa Shirika hilo wamekuwa wakionekana kila mahali ambapo majanga hutokea, ikiwemo ajali, ugaidi, njaa na kadhalika.

Alitaja eneo lake la Wajir na pia Mandera kuwa baadhi ya sehemu ambazo zimefaidi pakubwa na misaada ya Shirika la Msalaba Mwekundu.

“Ukienda Wajir, Mandera, Lamu na sehemu zote zinazokumbwa na changamoto mbalimbali, watu wa kwanza kuwapata pale wakisaidia ni maafisa wa shirika la Msalaba Mwekundu. Wale wanaoingilia utendakazi wa shirika hilo hawana utu,” akasema Bw Abdisalan.

Alisema kama mmoja wa maafisa wa zamani wa Shirika la Msalaba Mwekundu, yeye anajua matatizo ambayo shirika hilo hukumbana nayo.