Rigathi Gachagua ataka Wachina wadhibitiwe
Na MWANGI MUIRURI
MBUNGE wa Mathira Rigathi Gachagua alisema Ijumaa kuwa serikali kupitia Wizara ya Usalama wa Ndani inafaa kuhakikisha Wachina wamesakamwa ili wakome kunyakua fursa za riziki zinazowafaa Wakenya.
Bw Nyoro aliteta kuwa raia wa Kichina wamekuwa na uhuru mwingi sana hapa nchini kiasi kwamba wanapatikana katika kila kona ya nchi wakichoma mahindi, wakichuuza mali za rejareja na pia wengine wakishiriki biashara ya uchukuzi wa bodaboda.
Alisema kuwa serikali inafaa kuwa ya kujituma kulinda nafasi za Wakenya wa kiwango cha chini za kiuchumi na hivyo basi raia hao wa kigeni warejeshwe kwao wakapambane na hali ya kiuchumi katika nafasi za kwao nyumbani.
“Waziri Fred Matiang’i na Katibu katika wizara, Karanja Kibicho badala ya kushinda afisini wanafaa wawe nyanjani wakilinda kazi za Wakenya zisinyakuliwe na Wachina,” akasema Gachagua.
Alisema kuwa ukadiriaji wake unabainisha kuwa hapa nchini hakufai kuwa na zaidi ya Wachina 300.
“Tunahitaji tu maafisa wa ubalozi, wahandisi wachache katika kandarasi za Kichina na wengine wachache tu wakiwa hapa nchini kwa vibali vya kikazi. Wengine wanafaa kuwa hapa tu nchini kama wanafunzi au watalii,” akasema.
Bw Gachagua akiwa Mjini Karatina alisema kuwa kunafaa kuwa na sheria za kushinikiza Wachina walio hapa nchini kushiriki kikamilifu ujenzi wa taifa hili.
“Wale ambao wamepewa kandarasi za kujenga miundombinu hapa nchini hawatufai kiuchumi. Huwa hawakodishi vyumba vya makazi kwa kuwa huishi katika karakana zao za ujenzi, wanakuza mboga zao katika karakana hizo na huagiza bidhaa zao za matumizi kutoka taifa lao,” akasema.
Ni katika msingi huo ambapo Bw Gachagua alisema ameandaa mswada wa bunge wa kuhakikisha ushirika wa raia wa kigeni katika nyanja ya riziki hapa nchini imezua masharti makali.
“Sheria ninayopendekeza ni kuwa raia wa kigeni asipewe kandarasi au nafasi ya kazi ambayo gharama ya kuifanya ni kati ya Sh1 milioni na Sh1 bilioni. Gharama ikizidi hiyo, ni lazima ishirikishwe Wakenya kwa asilimia 30,” akasema.
Mswada huo unalenga kubadilisha vipengele kadhaa vya sheria ya Public Procurement and Asset Disposal Act 2015 ili kukaza masharti ya raia wa kigeni kushiriki nafasi za riziki nchini.
Mrengo huo wa Dkt William Ruto ukifahamika kama Tangatanga umekuwa katika vita baridi na Matiang’I na Kibicho kwa msingi wa madai kuwa wanatumika na wapinzani wa urithi wa urais 2022 kuwazimia mwanya wa kuibuka washindi.
Ni hali ambayo imempata Dkt Ruto hivi majuzi akisuta wizara hiyo kuwa injumuisha “wazembe, wajinga na washenzi” akiapa kuwanyorosha akitumia nguvu zake za unaibu wa rais.