• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 6:50 AM
Ripoti ya upasuaji yaonyesha aliyekuwa mlinzi wa Kidero aliuawa kwa kupigwa

Ripoti ya upasuaji yaonyesha aliyekuwa mlinzi wa Kidero aliuawa kwa kupigwa

NA GEORGE ODIWUOR 

MLINZI wa aliyekuwa Gavana wa Nairobi Evans Kidero alifariki kwa majeraha mabaya ya ubongo na kuvuja damu nyingi – utathmini wa upasuaji umebaini.

Evans Okoda, 35, alikutwa amekufa karibu na nyumba yake ya kukodi mjini Oyugi baada ya kushiriki starehe na marafiki kwenye klabu moja ya burudani Alhamisi usiku.

Alipopatikana, baadhi ya vidole vilikuwa vimeng’olewa pamoja na ulimi. Uso wake pia ulikuwa umeharibiwa.

Upasuaji uliofanywa katika Hospitali ya Kaunti ndogo ya Rachuonyo ulifichua ubongo wake ulikuwa umejeruhiwa vibaya sana.

Kwa mujibu wa ripoti ya Dkt Tobias Ocholla, majeraha aliyopata marehemu yalisababishwa na kifaa kikali.

Okoda alionekana sana katika matukio ya kisiasa hasaa wakati wa uchaguzi wa ugavana 2022 akiwa mlinzi wa Dkt Kidero.

Chanzo cha kifo chake bado hakijabainika.

Kamanda wa Polisi wa Rachuonyo Kusini Lilies Wachira alisema uchunguzi umebaini kuwa marehemu aliondoka nyumbani kujishughulisha  mjini Oyugis kabla ya kuonekana kwenye baa baadaye.

Mara ya mwisho alionekana kwenye baa ya kienyeji.

Majirani walipigwa na butwaa walipoona mwili huo nje ya nyumba yake Ijumaa asubuhi.

Inaaminika kuwa huenda aliuliwa wakati mvua kubwa ilikuwa inanyesha.

“Mvua kubwa ilikuwa ikinyesha usiku na hakuna mtu aliyesikia kishindo wakati wa shambulio hilo,” Bi Wachira alisema.

Alisema wameanzisha uchunguzi kuhusu kifo cha Okoda.

“Hakuna anayejua chanzo cha kifo hicho na hakuna mtu alisikia vurugu wakati huo,” Bi Wachira alisema.

Mwili huo ulipelekwa katika hifadhi ya maiti ya hospitali ya kaunti ndogo ya Rachuonyo Kusini.

Kifo cha Okoda kiliibua wasiwasi uliochochea maandamano mjini Oyugis.

Dkt Kidero anaomba mamlaka husika kuchunguza kisa hicho na kushtaki watakaopatikana na hatia.

 “Okoda alikuwa mmoja wa walinzi wangu wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa 2022 na mauaji yake ya kikatili yamezua wingu la hofu. Kitendo hiki kiovu kimesikitisha wakazi wengi wa kaunti ya Homa Bay,” alisema Bw Kidero katika chapisho la mtandao wa kijamii wa Facebook.

TAFSIRI : LABAAN SHABAAN

  • Tags

You can share this post!

Mvua ilivyomsomba daktari na kuchochea stima kuua mwanamke...

Korti yakataa kuzima kesi za ushuru wa nyumba, yaamuru...

T L