Rufaa ya baba mnajisi yatupiliwa mbali
NA PHILIP MUYANGA
MWANAMUME aliyenajisi bintiye mwenye umri wa miaka tisa zaidi ya miaka kumi iliyopita, atasalia gerezani maisha, baada ya Mahakama ya Rufaa kutupilia mbali rufaa yake ya kupinga uamuzi wa Mahakama Kuu uliothibitisha hukumu yake.
Majaji wa Rufaa Asike Makhandia na Agnes Murgor, waliamua kuwa SK almaarufu kama B, ni baba wa mtoto ambaye rekodi ya kesi ilithibitisha aliumizwa sana na kitendo hicho.
“Alikuwa na umri wa miaka tisa tu wakati kosa hilo lilifanyika bila mama yake kuwepo, aliweka imani yake kwa mkataji rufaa kumpa malezi na ulinzi wa wazazi lakini alisaliti kwa kumnajisi bila huruma,” waliamua majaji.
Majaji hao walisema walizingatia uzito wa kosa hilo, umri wa mtoto na ukweli kwamba mkataji rufaa ni baba yake.
Mahakama hiyo iliridhika kwamba ushahidi ulipozingatiwa kwa jumla ulithibitisha mtoto huyo alinajisiwa na SK almaarufu B, babake.
Katika rufaa yake, mkataji rufaa alidai kuwa Mahakama Kuu ilishindwa kufahamu kwamba mwathiriwa aliruhusiwa kutoa ushahidi kupitia kwa msaidizi ilhali hakutangazwa kuwa shahidi asiye na uwezo.
SK almaarufu B pia alidai kuwa Mahakama Kuu ilikosa kupata kwamba utaratibu uliowekwa wa kumteua mlezi wa mtoto kama msaidizi mahakamani haukufuatwa na kwamba ilishindwa kutambua upande wa mashtaka haukuthibitisha kesi yake kwa viwango vinavyohitajika.