Habari MsetoSiasa

Rungu la Moi halitamtikisa Ruto Rift Valley – Mbunge

February 16th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

OSBORN MANYENGO na ONYANGO K’ONYANGO

MBUNGE mwandani wa Naibu wa Rais Dkt William Ruto amesisitiza kwamba mkondo wa kisiasa Rift Valley hautabadilika hata baada ya Seneta wa Baringo Gideon Moi kupewa rungu la babake, hayati rais mstaafu Daniel arap Moi.

Akihutubu wakati wa mazishi katika kijiji cha Masop-Kimoson, Mbunge wa Endebess Kaunti ya Trans Nzoia, Dkt Robert Pukose, alisema Dkt Ruto ataendelea kuwa kigogo mkuu wa kisiasa kwa jamii ya Wakalenjin.

Alisema Rais Uhuru Kenyatta ana deni la kisiasa ambalo anapaswa kulipa wakati wa uchaguzi mkuu ujao kwa Dkt Ruto.

Kulingana naye, Wakenya bado wanakumbuka ahadi alizotoa Rais Kenyatta wakati wa kampeni kwamba ataongoza kwa mihula miwili na kisha kumuunga mkono Ruto atakapostaafu.

Dkt Pukose alizidi kusema, rais ajaye atachaguliwa kwa kuzingatia rekodi ya maendeleo kwa Wakenya wala si kwa msingi wa kupokezwa rungu la uongozi.

Alisema kuwa uongozi haupeanwi kupitia kwa sherehe ya matanga jinsi ilivyofanyika akitaka jamii ya Kalenjin kupitia kwa wazee kuelezea wazi Wakenya mila na tamaduni za jamii.

“Hili Rungu la Nyayo alilopewa Gideon halitabadilisha mkondo wa kisiasa Rift Valley. Bado ni Dkt Ruto ndiye tunajua ni kiongozi wetu,” akasema.

Kwingineko, madiwani wa Kaunti ya Trans-Nzoia wametoa wito ripoti ya BBI iwafikie wananchi mashinani ili waisome wenyewe na kuelewa yaliyomo ndiposa wajiamulie wanavyotaka.

Hayo yamejiri huku wazee wa jamii ya Wakalenjin wakisema wameshindwa kupatanisha Dkt Ruto na Seneta Moi kwa sababu wote wawili wana majivuno ya kisiasa.

“Hawakusema hawataki kupatanishwa lakini walikataa kukutana nasi. Kila mmoja wao alianza kusema anashughulika na mambo yake,” akasema Mwenyekiti wa baraza hilo linalofahamika kama Myoot, Bw John Seii.

Kulingana na wazee hao, kifo cha Mzee Moi kimeacha pengo ambalo sasa linatarajiwa kuzidisha mvutano kati ya wanasiasa hao wawili kuhusu uongozi wa kisiasa Rift Valley.

Katika mazishi aliyohudhuria, Dkt Pukose alishtumu vikali vitendo vya mauaji vinavyoendelea kati ya wapenzi.

Alitaka utengezaji wa pombe haramu kukomeshwa kabisa. Alisema kuwa marehemu aliuawa na mumewe, jambo ambalo lilichangiwa na ulevi.