Habari Mseto

Ruto aanza Ziara Rasmi ya Kitaifa Amerika ambayo Uhuru hakutunukiwa

May 20th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

JUSTUS OCHIENG NA KEVIN CHERUIYOT

RAIS William Ruto aliondoka nchini Jumapili usiku kwa safari yake ya kihistoria nchini Amerika.

Ziara hiyo inayotarajiwa kuwezesha mabadiliko makubwa kwa taifa, inalenga kuimarisha uhusiano kati ya mataifa hayo mawili.

Ziara hiyo ya kwanza kwa kiongozi wa Afrika katika kipindi cha miaka 15, itaanzia huko Atlanta. Hii, itakuwa ziara ya tatu pekee ya Kiserikali tangu Kenya kupata uhuru.

Ziara ya kwanza ilifanywa na Rais Daniel arap Moi mwaka 1980, ya pili na Rais Mwai Kibaki mwaka 2003.

Kulingana na Msemaji wa Ikulu Bw Hussein Mohamed, ratiba ya Rais Ruto nchini humo itaangazia ushirikiano wa miongo sita kati ya nchi hizo mbili. Na inatarajiwa kuvutia mikataba kadhaa.

Mnamo Jumatatu, Rais Ruto amepangiwa kutembelea Maktaba na Makumbusho ya Jimmy Carter huko Atlanta, Georgia, ambayo ni nyumba ya nyenzo za Rais Jimmy Carter inayohusishwa na utawala wa Carter kama Rais wa 39 wa Amerika.

Baadaye, Rais na mkewe, Bi Rachel Ruto watatembelea kanisa la Ebenezer Baptist, ambapo watatoa heshima kwa mapambano ya haki za raia.

“Atatoa heshima kwa mapambano ya haki za kiraia na kusisitiza jinsi dini inaweza kuwa nguvu ya wema. Ziara hii itasisitiza mapambano ya kihistoria ya usawa na haki,” alisema Bw Mohamed.