• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 9:37 AM
Ruto agomea mbio za Beyond Zero kwa mara ya kwanza

Ruto agomea mbio za Beyond Zero kwa mara ya kwanza

Na LEONARD ONYANGO

NAIBU wa Rais William Ruto Jumapili alikosa kushiriki makala ya tano ya mbio za Beyond Zero ambazo huandaliwa na mkewe Rais, Bi Margaret Kenyatta.

Naibu Rais Dkt William Ruto alikosa mbio hizo kwa mara ya kwanza tangu kuzinduliwa kwake mnamo 2014.

Badala yake, Dkt Ruto alienda katika eneo la Buuri, Kaunti ya Meru ambapo alihudhuria ibada kwenye Kanisa Katoliki, Parokia ya Kibirichia alipoendelea kukashifu watumishi wa umma anaodai wanajihusisha katika siasa za kumwekea visiki kwenye azimio lake la urais.

Mkewe Naibu wa Rais Rachel Ruto ambaye amekuwa akikimbia na Bi Kenyatta tangu 2014 pia hakujitokeza kushiriki mbio za jana.

Jana, Rais Kenyatta alipokelewa na mkewe Bi Margaret Kenyatta alipokamilisha mbio za umbali wa kilomita 2.

Mbio hizo za Nusu Marathoni zililenga kuchangisha fedha kwa ajili ya kuboresha afya ya akina mama wajawazito na kukabiliana na ukeketaji.

“Leo tumekimbia kwa sababu mbalimbali, tumekimbia kukabiliana na ukeketaji, kukabiliana na vifo wakati wa kujifungua, kupambana na maradhi ya fistula na kukemea ndoa za mapema miongoni mwa wasichana,” akasema Bi Margaret Kenyatta.

Baada ya kushiriki mbio za Beyond Zero, Rais Kenyatta alielekea uwanjani Kasarani kwa mechi baina ya Gor Mahia na AFC Leopards.

Rais Kenyatta aliandamana na kiongozi wa ODM Raila Odinga na mwenzake wa Amani National Congress (ANC) Musalia Mudavadi kati ya wengine.

Kwa upande mwingine, Dkt Ruto alitumia mitandao ya kijamii kuwatakia heri njema wanawake.

“Tutaendelea kuhakikisha wanawake wanawezeshwa kiuchumi, kuna usawa wa kijinsia na kuondoa ubaguzi dhidi yao. Wanawake ni muhimu katika kudumisha amani na ustawi wa maendeleo katika jamii yetu. Nawatakieni heri wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani,” akasema Dkt Ruto.

Katika mbio za Beyond Zero za mwaka uliopita, Dkt Ruto alitumia muda wa saa 2:4:12 kukimbia umbali wa kilomita 21 na alipokelewa kwa bashasha na Rais Uhuru Kenyatta aliyekuwa akimngojea katika mstari wa mwisho. Naibu wa Rais alikimbia kilomita 21 bila kusimama wala kutembea.

You can share this post!

Handisheki bila matunda

Kizazi kipya cha ‘Mamba’ kitamzuia Raila kufika...

adminleo