Habari Mseto

Ruto ajitosa mazima kwa mzozo wa ardhi ya Del Monte

February 17th, 2024 1 min read

NA MWANGI MUIRURI

MATAMSHI ya Rais William Ruto kwamba serikali yake itatoa hatimiliki kwa wanaonufaika kupata ardhi inayomilikiwa na kampuni ya Del Monte kutoka Marekani, yamesababisha hali kuwa tete.

Akizungumza katika Kaunti ya Murang’a mnamo Alhamisi, Rais Ruto alisema “tutatoa hatimiliki kwa wakazi ili wapate mashamba ambayo kampuni hiyo itawaachia”.

Mzozo unaozingira ardhi ya Del Monte umechochewa na kutokuwa tayari kwa taasisi na mamlaka husika kutangaza ekari halisi kampuni hiyo inayokuza mananasi inamiliki.

Mjadala kuhusu mashamba hayo ulianza pale Chama cha Wakazi wa Kandara kupitia ombi la Katibu Mkuu wake, Bw Geoffrey Kairu, kiliweka sehemu hizo za ardhi ya Del Monte kuwa mali yao lakini ilichukuliwa kwa nguvu na kukodishwa kwa kampuni hiyo na watu binafsi wasio waaminifu.

Ombi hilo kwa bunge na wanaharakati mashinani lilisababisha kufanyika kwa michakato kadhaa ya kutafuta ukweli.

Hadi sasa, hakuna mapatano yaliyofikiwa na wahusika wamehakikisha kuwa mjadala huo unakosa idadi madhubuti ya kufanya maamuzi.

Alipofika mbele ya kamati ya ardhi mnamo Mei 2022, aliyekuwa Waziri wa Ardhi Farida Karoney alisema serikali ilikusudia kurejesha ukodishaji wa ardhi hiyo kwa kampuni hiyo yenye ukubwa wa ekari 32,240.